G7 wataka wanajeshi wa Eritrea kuondoka Tigray | Matukio ya Afrika | DW | 02.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

TIGRAY

G7 wataka wanajeshi wa Eritrea kuondoka Tigray

Kundi la mataifa saba yanayoongoza kiuchumi limetaka wanajeshi wote wa Eritrea waliopo kaskazini mwa Ethiopia kuondoka, huku taasisi ya kimataifa ya kufuatilia migogoro (ICG) ikionya dhidi ya kuendelea kwa mkwamo.

Taarifa ya pamoja ya mawaziri wa mambo ya kigeni wa kundi la G7 iliyotolewa Ijumaa (Aprili 2) ilisema kwamba mchakato wa kuwaondowa wanajeshi hao lazima ufanyike kwa haraka.

"Tumelipokea tangazo la hivi karibuni la Waziri Mkuu Abiy Ahmed (wa Ethiopia) kwamba wanajeshi wa Eritrea wataondoka kutoka jimbo la Tigray. Mchakato huo lazima uwe wa haraka, usio masharti na unaoweza kuthibitishwa (kwamba unafanyika)." Lilisema tamko hilo lililotolewa mjini Berlin, Ujerumani.

Kiongozi wa muda wa jimbo hilo, Mulu Nega, aliliambia shirika la habari la AFP wiki hii kwamba suala la kuondoka kwa wanajeshi hao wa Eritrea ni mchakato ambao hauwezi kukamilika haraka. 

Wakaazi wa miji kadhaa ya Tigray waliiambia AFP kwamba hata baada ya kutolewa tangazo hilo la Waziri Mkuu Abiy, wanajeshi wa Eritrea wamezidi kujiimarisha kwenye baadhi ya maeneo. 

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mashahidi waliripoti kuyaona magari manne yakiwa yamejaa wanajeshi wa Eritrea yakiwasili kwenye mji wa Edaga Hamus.

Jinsi Eritrea ilivyojiingiza Ethiopia

Bildergalerie Äthiopien | Flucht aus der Region Tigray

Wakimbizi wa Tigray wakisubiri mgawo wa chakula katika mji wa Tsehaye.

Awali, serikali za Ethiopia na Eritrea zilikuwa zikikanusha kuwepo kwa wanajeshi wa Eritrea katika jimbo la Tigray, zikipingana  na ushahidi unaotolewa na wakaazi wa huko, makundi ya haki za binaadamu, wanadiplomasia na hata baadhi ya raia na maafisa wa kijeshi wa Ethiopia.

Abiy, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, alituma wanajeshi kwenye jimbo hilo la kaskazini mwa nchi yake mwezi Novemba 2020 kwa lengo la kuwatia nguvuni na kuwanyang'anya silaha viongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF), ambacho kiliwahi kulitawala jimbo hilo na, kwa hakika, Ethiopia nzima.

Wakati huo, waziri mkuu huyo alisema hatua iliyo ilikusudiwa kujibu uchokozi uliofanywa na TPLF kwa kuzishambulia kambi za jeshi la serikali ya shirikisho.

Licha ya Abiy kutangaza ushindi kwenye operesheni hiyo wiki chache baada ya kuanza, ukandamizaji umekuwa ukiendelea kwenye maeneo ya kati na kusini mwa Tigray, kwa mujibu wa kundi la ICG katika ripoti yake lilioichapisha siku ya Ijumaa (Aprili 2), ikiwa ni takribani miezi mitano tangu silaha ya kwanza risasi ya kwanza kusikika.

Mashirika ya haki za binaadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yanavituhumu vikosi vya Eritrea kwa mauaji ya kimbari dhidi ya mamia ya watu kwenye mji wa Axum jimboni Tigray yaliyotokea mwezi Novemba, huku shirika la habari la AFP likiripoti kuhusu mauaji mengine ya kimbari yaliyofanywa na wanajeshi hao wa Eritrea kwenye mji wa Dengolat.