FIFA yasisitiza Urusi itaandaa Kombe la Dunia | Michezo | DW | 25.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

FIFA yasisitiza Urusi itaandaa Kombe la Dunia

Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA limepinga wito wa kulitaka lihamishe dimba la Kombe la Dunia mwaka wa 2018 kutzoka Urusi, likisema kuwa kinyang'anyiro hicho “kinaweza kuleta mabadiliko makubwa”.

Madai kuwa Urusi ilihusika katika janga la kudunguliwa ndege ya abiria ya Malaysia katika anga ya Ukraine yalizusha wito kutoka kwa baadhi ya wabunge nchini Ujerumani wa kutaka uamuzi wa Urusi kupewa haki ya kuandaa fainali hizo utathminiwe upya. FIFA imetoa taarifa jana ikisema “linapinga aina yoyote ya machafuko” na inaunga mkono mdahalo wa amani na demokrasia pekee kuhusu Kombe la Dunia.

Shirikisho hilo linasema historia kufikia sasa inaonyesha kuwa kususia matamasha ya michezo au sera ya kutenga au mapambano siyo njia bora za kutatua matatizo. Badala yake Kombe la Dunia linaweza kutumiwa kama kitu kinachoweza kuchochea mazungumzo mwafaka baina ya watu na serikali husika.

Wakati huo huo, Wachezaji watatu wa kigeni wameripotiwa kuihama klabu ya Ukraine ya Volyn Lutsk wakati uasi ukiondelea katika eneo hilo la kusini mashariki. Wachezaji hao wametajwa kuwa ni Mromania Eric Bicfalvi, kiungo wa Brazil Ramon Lopes na mshambuliaji wa Nigeria Michel Babatunde.

Wiki iliyopita, wachezaji saba wa kigeni walikataa kurejea katika timu zao za Ukraine, Shakhtar Donetsk na Metalist Kharkiv kufuatia janga la kudunguliwa ndege ya abiria ya Malaysia. Klabu nyingine ya Ukraine Dynamo Kiev imeelezea matumaini kuwa itaweza kubakia na wachezaji wake wa kigeni.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef