FIFA yampiga marufuku Beckenbauer | Michezo | DW | 14.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

FIFA yampiga marufuku Beckenbauer

Kocha na nahodha wa zamani aliyeipatia ushindi wa Kombe la Dunia Ujerumani Franz Beckenbauer amepigwa marufuku kwa siku 90 kujihusisha na soka kwa kushindwa kutowa ushikiano wake kwa kamati ya uchunguzi ya FIFA.

Mwenyekiti wa heshima wa Bayern Munich Franz Beckenbauer.

Mwenyekiti wa heshima wa Bayern Munich Franz Beckenbauer.

Taarifa ya FIFA imesema Beckenbauer ambaye alikuwamo kwenye kamati kuu ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Soka (FIFA) ambayo hapo mwaka 2010 iliwapatia Qatar haki za kuwa mwenyeji wa michuano ya soka ya Kombe la Dunia kwa mwaka 2022,aliombwa mara kadhaa kutowa maelezo yake kuhusu uamuzi huo tata.

Marufuku hiyo imewekwa kufuatia ombi la mwanasheria wa Marekani Michael Garcia mkuu wa jopo la uchunguzi wa kamati ya maadili ya FIFA ambaye anaongoza uchunguzi kuhusu uamuzi huo wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022.

Hapo Jumatano Garcia aliuambia mkutano mkuu wa FIFA wa kila mwaka mjini Sau Paulo Brazil kwamba yeye na kamati yake tayari walikuwa na sehemu kubwa ya mamilioni ya nyaraka ambazo zimetajwa na gazeti la Sunday Times la Uingereza katika repoti ya karibuni inayodai kutolewa kwa rushwa katika harakati za kufanikisha Qatar ipate nafasi ya kuandaa michuano hiyo ya soka Kombe la Dunia.

Kukiuka maadili

Michael Garcia Mkuu wa Kamati ya Uchunguzi ya Maadili ya FIFA.

Michael Garcia Mkuu wa Kamati ya Uchunguzi ya Maadili ya FIFA.

Taarifa hiyo ya FIFA imesema "Franz Beckenbauer leo Jumamosi (13.06.2014)amepigwa marufuku kwa muda kushiriki katika shughuli zozote zinazohusiana na soka katika ngazi yoyote ile kwa siku 90." Imeongeza kusema kwamba marufuku hiyo inaanza kazi mara moja na kwamba uamuzi huo umechukuliwa kwa misingi ya kukiukwa kwa Kanuni za Maadili kunakoonekana kuwa kumetokea na kwamba uamuzi wa suala hilo yumkini ukawa haukuchukuliwa na mapema inavyostahiki.

Taarifa imeendelea kusema kwamba ukiukaji huo unaonekana kuhusiana na kushindwa kwa Bw.Beckenbauer kutowa ushirikiano wake kwa uchunguzi wa Kamati ya Maadili licha ya kuombwa mara kadhaa atowe msaada wake yakiwemo maombi yanayomtaka atowe maelezo wakati wa mahojiano ya na ana kwa ana au ajibu masuali ya maadishi yaliyotolewa kwa lugha zote mbili Kingereza na Kijerumani.

Alipoulizwa na kituo cha Televisheni cha Sky nchini Ujerumani hapo Ijumaa kwa nini amepigwa marufuku Beckenbauer amesema "Kwa kweli sijuwi kwa nini.Kitu cha kwanza nilichofanya ni kuangalia tarehe kwani nilidhani ulikuwa ni mzaha wa siku ya wajinga -April Fool".

Safari ya Brazil yafutwa

Franz Beckenbauer wa mwisho akiwa na timu ya Bayern Munich 1970.

Franz Beckenbauer wa mwisho akiwa na timu ya Bayern Munich 1970.

Akizungumza na gazeti litolewalo kila siku la Ujerumani la Bild hapo Jumamosi Beckenbauer mwenye umri wa miaka 68 ambaye alishiriki katika kulinyakuwa Kombe la Dunia akiwa mchezaji hapo mwaka 1974 na akiwa kocha hapo mwaka 1990 amesema anafuta safari yake ya kwenda Brazil kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwani haoni kama atakaribishwa baada ya FIFA kutangaza marufuku hiyo.

Marufuku dhidi ya Beckenbauer kwa kiasi kikubwa ni ya kiishara kwani hivi sasa sio tena mjumbe wa kamati kuu ya FIFA na hana dhima hasa katika kambumbu la Ujerumani ziada ya kuwa mwenyekiti wa heshima ya klabu ya Bayern Munich mabingwa wa Ujerumani.

Hata hivyo kutokana na rekodi yake ya uchezaji na ukocha na dhima yake akiwa kama mwenyekiti wa kamati iliyoandaa michuano ya Kombe la Dunia nchini Ujerumani hapo mwaka 2006 anaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika kabumbu la kimataifa.

Kikwazo cha lugha

Mwenyekiti wa heshima wa Bayern Munich Franz Beckenbauer.

Mwenyekiti wa heshima wa Bayern Munich Franz Beckenbauer.

Katika mahojiano na gazeti hilo la Bild Beckenbauer amesema hana kitu cha kuficha lakini amelalamika kwamba Garcia alikataa kuyaweka masuali yake katika lugha anayoifahamu.

Ameliambia Bild "Sina chochote kile cha kuficha na pia nataka ifahamike wazi kwamba lazima kuweko na vikwazo kwa wahusika pale inapothibitika kuwepo rushwa."

Amesema alikuwa tayari kujibu masuali yote yanayopaswa lakini walimtumia katika lugha ya kisheria ya Kingereza ambayo alishindwa kuyafahamu katika kesi ngumu kama hiyo.

Amesema aliomba kwa upole mahojiano hayo yafanyike kwa Kijerumani na alikataliwa.Pia amesema ana haki ya kuiweka siri kura yake FIFA ya mwaka 2010.

Lakini ameongeza kusema kwamba watu wenye kumbukumbu watakumbuka kwamba alitamka baada ya kura hiyo kwamba kuchaguliwa kwa Qatar kulimshtuwa na alikuwa wa kwanza kusema kwamba kufanya michuano ya Kombe la Dunia nchini humo ni jambo lisilowezekana na kwamba inabidi ifanyike majira ya baridi.

Harufu ya rushwa

Mohamed Bin Hammam mjumbe wa zamani wa kamati kuu ya FIFA.

Mohamed Bin Hammam mjumbe wa zamani wa kamati kuu ya FIFA.

Kwa mujibu wa repoti za vyombo vya habari vya Uingereza vikikariri maelfu ya baruwa pepe kuhusiana na kadhia hiyo Beckenbauer alikwenda Qatar akiwa mgeni wa Mohamed bin Hammam kabla ya ya kura hiyo ya mwaka 2010 na kukutana na Emir wa taifa hilo. Vimeongeza kusema kwamba alirudi tena nchini humo baada ya kupigwa kwa kura hiyo.

Gazeti la Sunday Times limesema baadhi ya mamilioni ya nyaraka imeziona kuwa zinahusiana na malipo yaliyotolewa na mjumbe wa zamani wa kamati kuu ya FIFA Bin Hammam kwa maafisa ikiwa kama sehemu ya kampeni ya kuungwa mkono kwa harakati za Qatar kuandaa michuano hiyo ya Kombe la Dunia.

Kesi hiyo hivi sasa iko kwenye taratibu rasmi za uchunguzi chini ya mjumbe wa jopo hilo Vanessa Allard akiwa kama mkuu wa uchunguzi.Repoti rasmi ya uchunguzi huo inatarajiwa kutolewa hapo mwezi wa Julai.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Oummilkher Hamidou