FIFA kumpata rais mpya Februari 26, 2016 | Michezo | DW | 20.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

FIFA kumpata rais mpya Februari 26, 2016

FIFA itaandaa uchaguzi maalum mnamo Februari 26 ili kuijaza nafasi ya rais Sepp Blatter. Hayo yametangazwa na shirikisho hilo la kandanda la kimataifa lililochafuliwa na kashfa ya rushwa

Hayo ni wakati aliyekuwa mwanakandanda nguli wa Ufaransa Michel Platini akikaribia kuzindua kampeni yake.

Kamati kuu ya FIFA wakiwemo Blatter na Platini, walikubaliana kuhusu tarehe hiyo kwenye mkutano mjini Zurich ambako mkutano maalum wa uchaguzi wa Baraza Kuu la FIFA utaandaliwa.

Blatter alitangaza mnamo Juni 2, siku nne baada ya kushinda muhula wa tano kama rais, kuwa atajiuzulu wakati wimbi kali la rushwa likilipiga shirika hilo la kandanda ulimwenguni.

Wagombea wa urais wa FIFA wana hadi Oktoba 26 kuwasilisha majina yao. Kufikia sasa, ni Zico, mcheza kandanda wa zamani wa Brazil aliyetangaza rasmi nia yake. Lakini rais wa Shirikisho la Kandanda la Ulaya – UEFA Michel Platini anapigiwa upatu kushinda ikiwa atagombea.

Schweiz, Sepp Blatter wird mit Geldscheinen beworfen

Sepp Blatter alitupiwa pesa bandia na mwandamanaji aliyeingia kisiri katika kikao cha wanahabari

Platini ataamua katika wiki mbili zijazo ikiwa atawania katika uchaguzi wa kumpata mrithi Blatter. Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 60, anatarajiwa kuwa anayeweza kushinda uchaguzi huo ikiwa atagombea. Duru imesema Platini anatafakari kutuma ombi baada ya kupata uthibitisho wa maneno kutoka kwa mashirkisho manne kati ya sita ya kikanda yanayounda shirikisho hilo la kandanda ulimwenguni. Ni shirikisho la kandanda Afrika – CAF na lile la Oceania ambayo hayamuungi mkono Platini.

FIFA imesema itaunda jopokazi la watu 11 litakalopendekeza mageuzi yanayolenga kulisafisha shirikisho hilo baada ya kukumbwa na msururu wa kashfa. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na viwango vya uadilifu kwa wanachama wa Kamati Kuu, kuanzishwa kwa ukomo wa mihula ya uongozi, viwango vya juu uongozi katika ngazi zote za miundo ya kandanda. Jopokazi hilo kisha litawasilisha ripoti yake kwa kamati kuu mwezi Seotemba, kabla ya kamati hiyo kuyapendekeza mageuzi hayo kwenye mkutano mkuu wa FIFA ambao una mamlaka ya kufanya marekebisho ya kisheria.

Na kuhusiana na suala hilo la mageuzi, kundi moja linalopigania mageuzi katika shirikisho hilo la kandanda la Kimataifa, limetoa wito wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kuongoza tume huru ya mageuzi.

Tim Noonan wa chama cha kimataifa cha wafanyakazi ITUC amesema shirika lake limewasiliana na Annan ambaye amewaambia kuwa yuko tayari kusikiliza ombi lolote kutoka kwa FIFA.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/APE/DPA/Reuters
Mhariri:Josephat Charo