1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Störung | WhatsApp, Facebook und Instagram
Picha: Ercin Erturk/AA/picture alliance

Facebook, WhatsApp, Instagram zarejea baada ya kuzimika

Saleh Mwanamilongo
5 Oktoba 2021

Mtandao wa Facebook na majukwaa yake ya yamerejea kufanya kazi baada ya kuzimika kote ulimwenguni kwa masaa kadhaa hali iliyoathiri biashara na huduma kadhaa.

https://p.dw.com/p/41H20

Tamko lililotolewa na uongozi wa Facebook baada ya kurejea huduma hiyo, limesema "chanzo cha kuzimika huko ni kosa la mabadiliko ya mitambo" na kwamba hakukuwa na ushahidi kuwa taarifa za watumiaji zimeathirika kutokana na tatizo hilo.

Kampuni hiyo imeomba radhi na kuahidi kuendeleza uchunguzi zaidi wa tukio hilo lililozua taharuki kote ulimwenguni.

Jake Williams, afisa mkuu wa ufundi wa kampuni ya usalama wa kimtandao BreachQuest, alisema kama hakukuwa na mchezo mchafu, basi tukio hilo linatokana na hitilafu za utendaji zilizosababishwa na makosa ya kibinadamu.

"Hakuna mtu aliye na kinga. Hakuna kampuni ambayo ina kinga kutokana na kukatika. Kwa hivyo wakati wote, wahandisi wanahitaji kufanya vitu kama hivi, wakitazama kampuni nyingine ambazo zimeathirika, kuelewa kwanini. Je! Hiyo ilitokeaje na ni vipi wanaweza kujifunza kutokana na hilo kuboresha michakato yao wenyewe? ", alisema Williams.

Soma pia:Facebook, Twitter zamlenga Trump 'kwa habari za kupotosha'

Wiki mbaya kwa kampuni ya Facebook

Mkurugenzi Mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg alipata pia pigo kubwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg alipata pia pigo kubwaPicha: Reuters/E. Scott

Hilo limejiri wakati Facebook ikiwa tayari kwenye mzozo mwengine mkubwa baada ya mvujisha siri Frances Haugen kulipatia jarida la Wall Street nyaraka zinazoonesha jinsi kampuni hiyo inavyofahamu madhara yanayosababishwa na huduma na maamuzi yake. Haugen, aliyekuwa meneja wa huduma wa Facebook, atatowa ushahidi mbele ya baraza la Seneti hivi leo.

Mbali na usumbufu kwa watu, wafanyabiashara na wengine ambao wanategemea huduma za kampuni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg alipata pia pigo kubwa kufuatia tukio la jana.

Tovuti ya ufuatiliaji wa mabilionea ya Fortune ilisema utajiri wa kibinafsi wa Zuckerberg umeporomoka kwa karibu dola bilioni sita kwa siku moja. Jumatatu, kampuni ya Facebook pia ilididimia kwenye soko la hisa kwa kupoteza asilimia 4.9.

Soma pia:Mtandao wa Facebook wazimwa Myanmar

Kukatika kwa kiwango hiki kwa muda mrefu ni nadra. Usumbufu mnamo 2019 uliacha Facebook na programu zake zingine kutoweza kufikiwa kote ulimwenguni kwa zaidi ya masaa 14. Kampuni nyingine kadhaa za teknolojia, ambazo ni pamoja na Reddit na Twitter, zilinufaika kutokana na shida hizo za Facebook, ambapo watumiaji wengi walikimbilia mitandao hiyo.