1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eritrea na Ethiopia zaandika Historia mpya

Saumu Mwasimba
14 Julai 2018

Rais wa Eritrea ameitembelea Ethiopia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili na kuandika historia mpya baada ya nchi mbili kumaliza vita vya muda mrefu

https://p.dw.com/p/31RvW
Äthiopien - Besuch des Präsidenten Isayas Afewerki aus Eritrea
Picha: Reuters/T. negeri

Rais wa Eritrea Isias Afwerki amesema historia imewekwa kufuatia ziara yake nchini Ethiopia Jumamosi. Hiyo ikiwa ni kauli yake ya kwanza katika ziara hiyo iliyokuja siku kadhaa baada ya nchi hizo mbili jirani kutangaza kumaliza vita. Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed naye akasema maneno hayawezi kuelezea furaha Waethiopia waliyokuwa nayo kwa sasa na kwamba historia inaandikwa wakati huu.

Katika hafla ya chakula cha mchana waziri mkuu huyo aliyemkaribisha kiongozi mwenzake amekumbusha juu ya kupotea kwa maisha ya watu lakini akasema kwamba wana bahati kuishuhudia siku hii ya kihistoria na yeyote atakayeisahau siku hii atakuwa haelewi hali ya watu wa nchi hiyo.

Eritrea - Der äthiopische Ministerpräsident Abiy und der eritreischen Staatschef Afewerki
Picha: Reuters/G. Musa Aron Visafric

Rais wa Eritrea Isaias Afwerki aliwasili mchana katika mji mkuu Addis Ababa kwa ziara ya siku tatu. Awali waziri wa habari wa Eritrea Yemane Meskel alithibitisha kuondoka kwa Rais Isias. Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ndiye aliyempokea katika uwanja wa ndege. Maelfu ya watu walijipanga katika barabara za mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa wakiwa wamevalia fulana zenye picha za viongozi wote wawili.

Bendera za nchi zote mbili zimeonekana zikipepea huku wengine wakipeperusha bendera kubwa za Eritrea. Wikendi iliyopita Waziri Mkuu wa Ethiopia alifanya ziara kama hiyo nchini Eritrea. Abiy mwenye umri wa miaka 42 ndiye aliyechukua hatua ya mwanzo mwezi uliopita kwa kuukumbatia kikamilifu mkataba wa amani uliofikisha mwisho vita vya mpakani vya kati ya mwaka 1998 hadi 2000 ambapo maelfu ya watu waliuwawa.

Äthiopien - Ankunft des Präsidenten Isayas Afewerki aus Eritrea
Picha: Reuters/T. Negeri

Ni ziara ya kwanza ya rais huyo wa Eretrea nchini Ethiopia kuwahi kufanya katika kipindi cha miaka 22.Eritrea itafungua ubalozio wake Ethiopia siku ya Jumatatu.  Shirika la kutetea haki za binadamu limetowa tamko wakati rais wa Eritrea alipowasili Ethiopia ambapo limeitaka nchi hiyo ambayo inakosolewa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu pamoja na kuwatia jela wakosoaji kuacha mara moja vitendo hivyo. Amnesty International limemtaka rais Afwerki kufungua ukurasa mpya wa kuheshimu haki za binadamu.

Mwandishi: Yusuf Saumu

Mhariri: Jacob Safari