1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Erdogan kupambana na wapinzani katika uchaguzi wa mitaa

Bruce Amani
31 Machi 2024

Waturuki wanapiga kura Jumapili katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaolenga jitihada za Rais Recep Tayyip Erdogan kuchukua tena udhibiti wa Istanbul kutoka kwa mpinzani Ekrem Imamoglu.

https://p.dw.com/p/4eIBV
Uchaguzi wa mitaa Uturuki
Erdogan anapambana kuchukua udhibiti wa Instanbul kutoka kwa mpinzani wake mkuu EmamogluPicha: John Wreford/SOPA Images/ZUMA Press Wire

Waturuki wanapiga kura Jumapili katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaolenga jitihada za Rais Recep Tayyip Erdogan kuchukua tena udhibiti wa Istanbul kutoka kwa mpinzani Ekrem Imamoglu, anayelenga kuurejesha upinzani kama nguvu ya kisiasa baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi wa mwaka wa 2023.

Meya wa Istanbul Imamoglu alimpa Erdogan na chama chake cha AK kipigo kikubwa kuwahi kushuhudiwa katika miongo miwili madarakani kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa 2019. Rais huyo alirejea tena mwaka wa 2023 kwa kuchaguliwa tena na wingi wa viti bungeni na washirika wake wa siasa kali za kizalendo.

Matokeo ya leo huenda yakaimarisha udhibiti wa Erdogan kwa Uturuki ambayo ni mwanachama huyo wa Jumuiya ya Kujihami NATO, au kuashiria mabadiliko katika mazingira yaliyogawanyika katika dola hilo kubwa linaloibukia kiuchumi. Ushindi wa Imamoglu unaonekana kuchochea matarajio ya yeye kuwa kiongozi wa siku zijazo wa kitaifa.

Karibu watu milioni 63 wana haki ya kupiga kura kuwachagua mameya katika miji 81 ya Kituruki na manispaa. Wachambuzi wanasema uchaguzi huo wa leo ni muhimu kwa vyama vya upinzani nchini humo, ambavyo viko chini ya kitisho cha kutengwa kabisa na utawala unaozidi kuwa wa kimabavu.