Erdogan ameshinda urais Uturuki | Matukio ya Afrika | DW | 24.06.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Erdogan ameshinda urais Uturuki

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameshinda uchaguzi wa rais (24.06.2018) kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa leo na baraza la kitaifa la uchaguzi.

Wapiga kura kwa mara ya kwanza walipiga kura kumchagua rais na bunge katika uchaguzi wa mapema, huku Erdogan akitafuta ushindi katika duru ya kwanza na wingi wa wajumbe wa chama chake kinachotawala cha Haki na Maendeleo, Justic and Development, AKP.

Ushindani ulikuwa mkubwa katika uchaguzi huu hususan ikizingatiwa rais mpya ndiye wa kwanza kufurahia mamlaka yaliyoimarishwa chini ya katiba mpya iliyoridhiniwa kupitia kura ya maoni iliyofanyika Aprili 2017, ambayo iliungwa mkono sana na rais Erdogan.

Matokeo yaliyotangazwa mapema leo Jumatatu na baraza la kitaifa la uchaguzi yanaonesha kwamba Erdogan amemshinda mpinzani wake wa karibu Muharrem Ince kwa zaidi ya nusu ya kura pasipo kuhitaji duru ya pili. Matokeo haya yametangazwa baada ya Erdoga kujitangaza mshindi.

"Matokeo yasiyo rasmi yamebainika. Kulingana na matokeo haya nimepewa dhamana na taifa na kutwikwa majukumu ya rais," Erdogan alisema katika makazi yake mjini Istanbul. Rais huyo wa Uturuki aidha alisema muungano unaongozwa na chama cha AKP umeshinda wingi wa wajumbe bungeni.

Erdogan amepata asilimia 52.5 ya kura za urais huku Ince wa chama cha Republican People, CHP akijikingia asilimia 31, limesema shirika la habari la serikali, baada ya jumla ya asilimia 97.7 ya kura zote kuhesabiwa. Takwimu hizi zinaweza kubadilika huku masunduku ya mwisho ya kura yakiendelea kuhesabiwa, lakini kura hizi hazitaathiri matokeo.

Kwa mujibu wa waandishi wa habari wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, sherehe tayari zilianza nje ya makazi ya rais Erdogan mjini Istanbul na katika makao makuu ya chama cha AKP mjini Ankara, huku kadamnasi ya watu wakipeperusha bendera.

Wagombea wanaovuta mkia katika matokeo ya uchaguzi wa Jumapili ni Meral Aksener wa chama cha kizalendo cha Good Party kikiwa na asilimia zaidi ya saba ya kura na Selahattin Demirtas wa chama kinachoegemea upande wa Wakurdi cha People's Democratic, HDP, kikiwa na asilimia nane.

Mwandishi: Josephat Charo/afp/ape

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com