Erdogan aahidi ushirikiano wenye manufaa kwa Afrika | Matukio ya Afrika | DW | 19.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Erdogan aahidi ushirikiano wenye manufaa kwa Afrika

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan leo ameianza ziara yake ya mataifa matatu barani Afrika nchini Angola kwa kuyatuhumu mataifa ya magharibi kupuuza miito ya mabadiliko katika barani Afrika.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan leo Jumanne ameianza ziara yake ya mataifa matatu barani Afrika akianzia nchini Angola. Akizungumza mjini Luanda, Erdogan ameyatuhumu mataifa ya magharibi kwa kupuuza miito ya mabadiliko katika barani Afrika.

Tangu alipoingia madarakani karibu miongo miwili iliyopita akiwa kwanza kama waziri mkuu, rais huyo wa Uturuki amekuwa akikuza mahusiano na Afrika kwa kuionesha nchi yake kuwa mshirika bora kuliko watawala wa zamani wa bara hilo pamoja na China.

Kwa mujibu wa taarifa ya chama chake cha AK, Erdogan wakati akizungumza na viongozi wa biashara katika mkutano mjini Luanda jana jioni  alisema, Uturuki inatoa umuhimu mkubwa na kuthamini uhusiano wake wa karibu na bara la Afrika, na kwamba wanatamani kuendeleza mahusiano katika misingi ya kunufaisha pande zote kwa usawa na kuheshimiana.

Awali katika hotuba yake kwa bunge la Angola iliyochapishwa katika tovuti ya Rais ya Uturuki, Erdogan alisema, hatma ya ubinadamu haiwezi na haipaswi kuachwa mikononi mwa huruma ya kundi la mataifa ambayo yalikuwa washindi wa vita ya pili ya dunia. Aliongeza kuwa kupuuza matakwa ya mabadiliko ni udhalimu kwa bara la Afrika. Alibainisha kuwa Uturuki haikuwa na "doa" la ubeberu au ukoloni na ilikataa mitizamo ya  "kimagharibi  kwa bara la Afrika''

Gesi asilia yawa sehemu ya mazungumzo

Akizungumza na mwenzake wa Angola Joao Laurenco, alizungumzia hifadhi za gesi asilia ya Uturuki na mtandao wa usambazaji ambapo alieleza kwamba atafurahi kubadilishana uzoefu na taifa hilo. Erdogan anatarajiwa kuelekea Togo baada ya Angola na kisha anatarajiwa kuelekea katika Taifa lenye nguvi kiuchumi barani Afrika la Nigeria.

Angola | Recep Tayyip Erdogan trifft Joao Manuel Goncalves Lourenco

Marais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Joao Lourenco wa Angola na wake zao

Kabla ya kufika Angola, Rais Recep Tayyip Erdogam, alishafanya ziara 38 katika mataifa 28 tangu alipokuwa waziri mkuu mnamo mwaka 2003. Uturuki ina balozi 43 barani humo na shirika lake la ndege la taifa linatoa huduma zake kwa zaidi ya miji 60 ya bara la Afrika. Hi ni pamoja na safari za ndege za moja kwa moja kati ya Luanda na Istanbul zilizozinduliwa wiki iliyopita.