1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS yaziondolea vikwazo Guinea, Mali

Sudi Mnette
26 Februari 2024

Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imetangaza kupunguza vikwazo dhidi ya Guinea na Mali, ikiwa ni siku moja baada ya kutangaza uamuzi kama huo kwa Niger.

https://p.dw.com/p/4csrM
Mkutano wa ECOWAS wa Nigeria mjini Abuja
Rais wa Tume ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, Omar Touray (kushoto) Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo (katikati) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yussuf Tuggar (kulia) wakati wa kikao cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi. (ECOWAS) Februari 24, 2024.Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Jumuiya hiyo iliweka vikwazo kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi hizo. Hatua zinazohusu Guinea na Mali, ambazo zilizoamuliwa Jumamosi, hazikutajwa wakati wa hotuba ya mwisho ya Mkuu wa Kamisheniya ECOWAS Omar Alieu Touray lakini zilionekana katika taarifa ya mwisho ya umoja huo.

Aidha Touray amesema mamlaka inataka kuachiliwa mara moja kwa Mohamed Bazoum, rais wa zamani wa Jamhuri ya Niger, zaidi alisema "Uamuzi huu unatokana na mazingatio ya kibinadamu, haswa tukiwa katika mwezi wa Kwarezma na tunapojiandaa kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani."

Rais Tinubu: ECOWAS kutafakari utaratibu wake wa kikatiba

Mkutano wa ECOWAS wa Nigeria mjini Abuja
Rais wa Nigeria na Mwenyekiti, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) Bola Tinubu, katika kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) mjini Abuja, Nigeria Februari 24, 2024. Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

ECOWAS ilichukua uamuzi wa kuzisimamisha nchi zote tatu na Burkina Faso kutoka katika uanachama wa umoja huo kwa sababu ya kufanya mapinduzi ya kijeshi. Mwanzoni mwa mkutano wa kilele wa Jumamosi, Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu amenukuliwa akisema lazima wangalie upya mtazamo wao wa sasa wa kutafuta utaratibu wa kikatiba katika nchi nne wanachama wao. Kwa sasa Nigeria inashikilia uenyekiti wa kupokezana kwa zamu wa ECOWAS.

Jumuiya hiyo ilipiga marufuku usafirishaji wa fedha wa  mwanachama wake Guinea baada ya Kanali Mamady Doumbouya kumuondoa kwa nguvu madarakani rais Alpha Conde mwaka 2021. Vikwazo vya kiuchumi na kibiashara dhidi ya Mali, ambayo ilifanya mapinduzi mwaka 2020 na 2021, viliondolewa mwaka 2022 baada ya jeshi kutangaza ratiba ya kurejea kwa utawala wa kiraia.

Baadhi ya vikwazo vilivyoondolewa dhidi ya mataifa yanayoongozwa kijeshi

Ruhusa ya safari za ndege, kufunguliwa mipaka na mali zilizozuiliwa dhidi ya Niger ni miongoni mwa hatua zilizoondolewa Jumamosi kwa "misingi ya kibinadamu", baada ya mapinduzi ya mwaka jana, ambayo yalimweka kando ya uongozi rais Mohamed Bazoum. Hata hivyo vile vikwazo vya kisiasa na vilivyowekwa kwa mtu mmoja mmoja bado vinaendelea.

Hatua ya ECOWAS inaashiria hamu ya kufanya upya mazungumzo na tawala za kijeshi miongoni mwa wanachama wake baada ya Mali, Niger na Burkina Faso kutangaza nia yao ya kuondoka katika umoja huo.

Soma zaidi:ECOWAS yatoa wito wa umoja

Nchi hizo tatu zimeunda muungano, zikakata uhusiano na mshirika wa jadi wa usalama Ufaransa na kuunda uhusiano wa karibu na Urusi, ambayo inatafuta ushawishi mkubwa barani Afrika.

Chanzo AFP