1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DW yasherehekea miaka 65

Zainab Aziz
5 Juni 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameahidi kuendelea kuliimarisha shirika la utangazaji la Ujerumani, DW. Bibi Merkel amesema hayo katika maadhimisho ya mwaka wa 65 tangu kuanzishwa kwa shirika hili la matangazo ya nje.

https://p.dw.com/p/2yyxf
Bundeskanzlerin Angela Merkel, DW-Intendant Peter Limbourg und Staatsministerin Prof. Monika Grütters, Beauftragte der Bundesregierung für Kultur und Medien, beim Festakt 65 Jahre DW
Picha: DW/J. Roehl

Kiongozi huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa chombo hiki cha habari kinatetea uhuru wa habari na uhuru wa maoni na amesisitiza kwamba katika nyakati hizi za taarifa bandia, ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kuwepo kwa kituo kama DW. Pia amesema kuwa idadi ya wabunge wanaosikiliza DW imeongezeka na kwa hivyo amemwambia Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter Limbourg kuwa anaweza kuwa na matumaini ya kuendelea  kupata uungwaji mkono wa kisiasa.

Bibi Merkel amesema thamani ya nchi ya Ujerumani inazidi kuongezeka ndani na katika bara la Ulaya. Amesema Ujerumani inachukuliwa kuwa ni mshirika muhimu. Kansela wa Ujerumani ameipongeza DW na kuongeza kwamba kuweka mtazamo wa Ulaya kwenye matukio ya ulimwenguni ni kazi mojawapo itakayokuwa muhimu zaidi. 

Katika hotuba yake ya maadhimisho hayo, Limbourg amezungumzia juu ya changamoto na malengo ya shirika lake na amesisitiza juu ya umuhimu wa shirika lake kuwezeshwa kifedha. 

Mkurugenzi mkuu wa DW Peter Limbourg
Mkurugenzi mkuu wa DW Peter LimbourgPicha: DW/J. Roehl

Bwana Limbourg amesema Deutsche Welle inawafikia watu wengi ulimwenguni kote tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Amesema ni shirika lililo na hadhi kubwa nchini Ujerumani miongoni mwa matabaka ya kisiasa. Amesisitiza kuongeza juhudi ili kuwapasha watu habari za kina hasa katika maeneo ambako uhuru wa vyombo vya habari unakandamizwa na kutawaliwa na propaganda na pia kuendelea kuitangaza Ujerumani na Ulaya kwa jumla.

Limbourg ametilia maanani kuwa ushindani duniani umezidi kuwa mkali na ameeleza kuwa teknolojia ya digitali inalazimu kutafuta majawabu mapya na vile vile uwepo wa madikteta katika sehemu mbalimbali za dunia unaifanya kazi iwe ngumu. Mkurugenzi huyo mkuu wa DW amesema hapana budi kutafuta njia mpya na amelitia maanani wazo la kituo kimoja cha televisheni cha Uturuki, la kulifanya jukumu la kulinda uhuru wa vyombo vya habari duniani kuwa jambo la thamani kwetu.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge inayoshughulikia masuala ya utamaduni na vyombo vya habari, Katrin Budde ameielezea DW kuwa sauti ya bunge la Ujerumani. Amesema shirika hili linatetea utangazaji wa habari za kweli na siyo za bandia. Budde pia amesisitiza kwamba katika nyakati hizi za kuongezeka kwa uzalendo wa kishabiki, ugaidi na propaganda, umuhimu wa DW umezidi kuwa mkubwa.

Mwandishi Zainab Aziz/DPAE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo