1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha Siku ya Idadi ya Watu

Lubega Emmanuel 11 Julai 2019

Duniani inaadhimisha siku ya idadi ya watu chini ya kauli mbiu ya ‘uzazi wa mpango ni haki ya binadamu’. Kauli mbiu hio inalenga kuhamasisha jamii na hususan familia kujenga uelewa juu upatikanaji wa huduma na matumizi ya njia mbalimbali za kupanga idadi ya watoto wanaoweza kuwazaa na kuwalea vyema.

https://p.dw.com/p/3LuOZ

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za shirika la Umoja Mataifa la Idadi ya Watu UNFPA inakadiriwa kuwa kuna zaidi ya watu bilioni 7.7 duniani. Idadi ambayo inaelezwa kukua kwa aslimia 1.2 kila mwaka ikimaanisha kuwa angalau kila dakika moja watu wawili wanazaliwa. Suali ni je kila anayezaliwa mimba yake huwa ilipangwa au haikupangwa na wazazi wake hasa mama yake? Hapo ndipo suala la haki za uzazi wa mpango linapochomoza. Hata hivyo kuna dhana kwamba suala la uzazi wa mpango limeeleweka vibaya kuhusiana idadi ya watoto.

Miongoni mwa watoto wanaozaliwa kinyume na nia ya mama yao ni pale mimba inapotokana na kunajisiwa au kubakwa pamoja na mimba za utotoni au kutokana na ndoa za lazima ambazo wakati mwingine msichana au mwanamke angependa kuwa na haki kuitoa. Hilo pia ni suala la haki katika uzazi wa mpango.

Kisha kuna ule mjadala ambapo katika mataifa fulani, mwanamke anaweza kumshtaki mumewe kwamba amembaka. Kuna maoni mbalimbali kuhusu suala hilo lakini madaktari wanashauri kuwa wakati mwingine hii hutokana na mienendo ya baadhi ya wanawake kuamua kutumia huduma za uzazi wa mpango bila kushauriana na mume. 

Tahadhari aidha inatolewa kwa vijana kutotumia kiholela aina fulani za kuzuia mimba kama njia yao ya uzazi wa mpango ambazo zaweza kuathiri afya yao, japo wana haki kuzitumia. Viongozi wa kidini nao wamehusika katika mjadala wa haki za uzazi wa mpango pale wanapowahimiza waumini kutoshiriki katika vitendo kama utoaji mimba au kutumia njia za kuzuia mimba.

Kuongozeka kwa kasi kwa idadi ya watu kunatajwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwa njia mojawapo ya kukuza uchumi wa nchi. Lakini wataalam wa kiuchumi wanaelezea kuwa hali hii ndiyo chanzo cha umasikini kuongezeka duniani kwani kasi hiyo hailingani na ukuaji wa kiuchumi na badala yake pia huchangia katika kuzorota kwa mazingira na uotoasili.