DRC: Nchi hatari zaidi kwa mama | Matukio ya Afrika | DW | 07.05.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

DRC: Nchi hatari zaidi kwa mama

Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto - Save the Children limeitaja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuwa eneo baya zaidi ulimwenguni kuishi ukiwa mama, wakati Finland ikiibuka eneo bora zaidi.

Wanawake wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo

Wanawake wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo

Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto - Save the Children limeitaja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuwa eneo baya zaidi ulimwenguni kuishi ukiwa mama.

Ripoti ya shirika hilo lenye makao yake jijini London Uingereza iliyotolewa leo inaonyesha kuwa mataifa ya kiafrika yemechukua nafasi zote kumi za chini kabisaa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 14 wakati Finland na nchi nyengine za Skandinavia zikiongoza katika kumi bora.

Nembo ya shirika la Save the Children

Nembo ya shirika la Save the Children

Ripoti hiyo iliyopewa kichwa cha 'Hali ya kina mama wa dunia' inalinganisha mataifa 176 kwa kuizingatia vitu kama afya ya uzazi, vifo vya watoto, elimu na viwango vya mapato ya wanawake na hadhi zao za kisiasa. Save the Children ilitoa wito wa kupunguza tofauti kubwa katika upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi kati ya mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea, na kuwepo na juhudi za maksudi kupambana dhidi ya ukosefu wa usawa na utapiamlo.

Ripoti hiyo imegundua kuwa mwanamke au msichana yuko katika hatari zaidi ya kufariki kutokana sababu zinazohusiana na uzazi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa nafasi moja katika 30, hii ikiwa ni pamoja na wakati wa kujifungua, ikilinganishwa na nchini Finland, ambako hatari hiyo ni nfasi moja katika 12,200. Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Save the Children Jasmine Whitehead, alisema kwa kuwekeza kwa kina mama na watoto, mataifa yatakuwa yanawekeza katika mafanikio yao ya baadae.

Elimu kwa wanawake itasaidia ustawi wao na wa watoto

Amesema kama wanawake wanaelimishwa, wanawakilishwa kisiasa, na wanapata huduma nzuri za afya ya uzazi na huduma za watoto, basi kuna uwezekano mkubwa kwa wao na watoto wao kuishi vizuri na kustawi , na hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa jamii wanamoishi. Alisema kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mataifa yanaoyoendelea, lakini kazi bado kuna kazi kubwa inayotakiwa kufanywa ili kuokoa na kuboresha mamilioni ya maisha ya kina mama maskini zaidi na ya watoto wanaozaliwa.

Wanawake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wakisubiri maji mjini Kinshasa.

Wanawake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wakisubiri maji mjini Kinshasa.

Baada ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, mataifa yanayofuatia kwa kuwa hatari zaidi kwa kina mama yaliorodheshwa kuwa ni Somalia, Sierra Leon, Mali na Niger. Ripoti hiyo inasema viwango vikubwa vya vifo vya watoto katika bara la Afrika chini ya jangwa la Sahara, vinatokana na afya duni ya kina mama -- ikionyesha tarakimu zinazoonyesha kuwa asilimia kati ya 10 na 20 wako chini ya uzito unaotakiwa.

Ripoti hiyo pia ilitoa umuhimu kwa idadi ya kina mama wanaojifungua kabla watoto wao hawajakua, matumizi madogo ya vizuia mimba, upatikanaji mdogo wa huduma za afya ya uzazi na uhaba wa wafanyakazi wa afya. Mataifa ya juu baada ya Finland ni Sweden, Norway, Iceland na Uholanzi, wakati Marekani ikishika nafasi ya 30 nyuma ya Slovenia na Lithuania.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman