1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund na PSG zatinga nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya

Bruce Amani
17 Aprili 2024

Borussia Dortmund na Paris Saint-Germain zimejikatia tiketi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya zote kupata ushindi katika mechi zao za kukata na shoka dhidi ya Atletico Madrid na Barcelona.

https://p.dw.com/p/4erkJ
Ian Maatsen akisherehekea bao lake dhidi ya Atletico Madrid
Hii ni mara ya kwanza tangu msimu wa 2012-13 walipopoteza fainali dhidi ya Bayern, kwa Dortmund kutinga nusu fainaliPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Dortmund iliizaba Atletico Madrid 4 – 2 na kufuzu kwa jumla ya mabao 5-4, wakati PSG ilipambana na kushinda 4-1 dhidi ya Barcelona iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani na hivyo kufuzu kwa jumla ya mabao 6 - 4.

Soma pia: Dortmund na PSV walitoka sare nchini Uholanzi

Hii ni mara ya kwanza tangu msimu wa 2012-13, wakati walipopoteza fainali dhidi ya Bayern Munich, kwa Dortmund kufika nusu fainali. Kocha wa Dortmund Edin Terzic anahisi kuwa timu yake, ambayo ilishinda Ligi ya Mabingwa mwaka wa 1997, sasa imejiandaa vizuri kuwakabili mabingwa hao wa Ufaransa, baada ya Wajerumani hao kupoteza mechi ya ugenini na kutoka sare nyumbani katika hatua ya makundi msimu huu.

Katika mechi za leo, Real Madrid wanakaribishwa nchini Uingereza kuangushana na Manchester City wakati matokeo ya mechi ya kwanza yakiwa 3 – 3. Nao Bayern Munich wanawaalika Arsenal dimbani Allianz Arena. Mechi ya kwanza ilikamilika kwa sare ya 2 – 2.