Dola la Kiislamu ladukuliwa mtandaoni | Masuala ya Jamii | DW | 18.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Dola la Kiislamu ladukuliwa mtandaoni

Kundi la wadukuzi "hackers" la Anonymous limeapa kutokomeza akaunti za Dola la Kiislamu kwene mitandao ya kijamii. Akaunti hizo za Facebook na Twitter zinatumika kusambaza propaganda.

Kufuatia kundi la dola la kiislam kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kufanya propanganda ikiwepo kuwapata na kuwaajiri wapiganaji wake, kundi hilo sasa huenda likafika mwisho wa propaganda zake.

Hali hiyo inafuatia kuwepo kwa kundi lingine linalojulikana kama Anonymous ambalo linaingia katika kurasa za mitandao ya kijamii za IS na kuziteketeza taarifa zinazotolewa na kundi hilo. Kundi hilo la wadukuzi wa mitandao linalojiita kwa Kiingereza Anonymous yaani "wasiojulikana" tayari limefuta maelfu ya akaunti za mtandao wa Twitter zilizoanzishwa kwa lengo la kuunga mkono kundi la IS.

Maelfu ya akaunti za twitter za IS zafutwa

Akaunti ya Twitter ene propaganda za Dola la Kiislamu

Akaunti ya Twitter ene propaganda za Dola la Kiislamu

Anonymous lilidai siku ya jumanne kuwa lilizifuta akaunti 5,500 za Twitter zinazohusishwa na kundi la Islamic state ambao walihusika na mashambulizi ya Paris, mwishoni mwa wiki iliyopita. Kundi hilo lilitoa madai hayo kupitia mtandao wa twitter siku moja baada ya kuanzishwa kwake, ambapo lilianza kampeni kupitia mtandao waliyoiita #OpParis kwa maana ya operesheni paris, ikiwa na lengo la kuzuia kampeni, shughuli zote za zinazofanywa IS kupitia mitandao ya kijamii.

Wadukuzi hao, hapo jumatatu walituma ujumbe katika mtandao wa twitter uliosema "Tunatoa taarifa kuwa zaidi ya akaunti 5,500 za Twitter za IS sasa zimefutilliwa mbali.” ujumbe huo uliambatana na ujumbe wa picha ya video. Hata hivyo bado haijawa wazi ni jinsi gani wameweza kuziondoa akaunti hizo za IS, lakini ujumbe mfupi uliotumwa na IS kwa njia ya Telegram ulitoa wito kwa kundi hilo kulinda mawasiliano yao ya mtandaoni.

Ujumbe huo ulisomeka kuwa “wadukuzi wa mtandao wanadukua harakati zetu na kuwataja kuwa ni wapumbavu.” Wakati kundi hilo Anonymous likiwa limeanza opereshi ya kufuta na kuziondoa harakati za kundi la IS katika mitandao ya kijamii, kundi lingine nalo limejitokeza na kudai kuwa wamekuwa wakifanya zaidi hilo kwa muda mrefu.

Kundi lingine nalo kuiunga mkono Anonymous

Vijana wengi wanaojiunga na Dola la Kiislamu wanasema wanafanya hivo kwa sababu ya kuvutiwa na wanachokiona mtandaoni

Vijana wengi wanaojiunga na Dola la Kiislamu wanasema wanafanya hivo kwa sababu ya kuvutiwa na wanachokiona mtandaoni

Kundi linalotoa taarifa kwa serikali ya Marekani limesema kuanzia Januari mwaka huu limefuta maelfu ya akaunti za Twitter zinazomilikiwa na IS na wanachama wake ikiwa ni harakati zake za kupambana na kile walichokiita operesheni ya mtadaoni ya kundi la IS na wanaounga mkono kundi hilo.

"Tunachukua jukumu la kijasusi zaidi,” alisema mkurugenzi wa kundi hilo ambalo limepachikwa jina la Ghost Security Group ambaye hakutaka kutaja jina lake. Mjumbe na mshauri wa masuala ya kigaidi, Michael Smith alisema kuwa kundi hilo limekuwa likitoa taarifa kwa shirika la kijasusi la Marekani FBI na mashirika mengine. Smith alisema juhudi za kundi hilo zimefanikisha kuchukuliwa kwa hatua muhimu na serikali hatua iliyopelekea kulalamikiwa kwa mtandao wa Twitter kuwasukumilia mbali watumiaji wa mtandao huo wanachama la kundi la IS.

Kampeni kuendelea katika mitandao mingine

Smith alisema mashirika ya kipelelezi ya Marekani yanathamini juhudi zinazofanyika nje ya taasisi na amekuwa akipata mrejesho wa mara kwa mara kuhusu hilo. Nae jenerali mstaafu David Petraeus hivi karibuni alikaririwa akisema kuwa taarifa zinazotolewa na kundi la Smith zinachukuliwa kuwa ni za muhimu na zinasaidia katika juhudi za kupambana na ugaidi.

Wakati kundi hilo la Anonymous na Ghost Security Group yakijitokeza kupambana na operesheni za IS kupitia mitandao ya kijamii, mtandao wa Facebook mwaka huu ulipiga marufuku aina yeyote ya kuunga mkono makundi ya kigaidi katika mtandao huo. Na kundi la udukuzi la Ghost Security Group limesema mtandao wa Youtube nao uko mbioni kuondoa video zote zinazoonesha mauaji.

Mwandishi: Mwazarau Mathola/RTRE/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com