1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dimbwi la Ondiri hatarini kutoweka

1 Februari 2019

Eneo chepechepe la Ondiri ni muhimu kwa wakazi wa mji wa Kikuyu na jiji la Nairobi nchini Kenya kwani ni vyanzo vya maji. Lakini sasa linakabiliwa na kitisho cha kuchafuka na kukauka.

https://p.dw.com/p/3CZLU
Kenia Nairobi Ondiri Sumpf
Vibanda vya mabomba ya maji yanayoyasambaza kwa wakazi wa Nairobi na KikuyuPicha: DW/Thelma Mwadzaya

Dimbwi la Ondiri ni la kipekee nchini Kenya kwani linatetema ukilikanyaga na unaporukaruka. Ondiri ni la pili kwa ukubwa barani Afrika ikilinganishwa na lililoko Douala,Cameroon. Hata hivyo liko katika hatari ya kukauka kwani maji yake yanafyonzwa kwa mabomba makubwa ili yakidhi mahitaji ya wakazi wa Kikuyu. Kadhalika shughuli za kilimo ukingoni mwa Ondiri pia zinachangia hali hiyo.

Mandhari ya kuvutia

Upepo na mazingira tulivu ndiyo yanayokulaki baada ya kushuka kwenye eneo la mteremko ulioko pembezoni mwa barabara kuu ya kusini mwa jiji la Nairobi. Dimbwi la Ondiri liko umbali wa kilomita moja kutokea mji wa Kikuyu katika kaunti ya Kiambu. Kwa mujibu wa wataalam wa maji na mazingira maji ya dimbwi hilo yana kina cha kilomita kumi. Manufaa yake ni maji ya matumizi, kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, na kuwa chanzo cha Mto Nairobi.

Kenia Nairobi Ondiri Sumpf
Nyasi na miti inayomea katiak dimbwi la Ondiri na mtoto akivuka upande wa piliPicha: DW/Thelma Mwadzaya

Sam Dindi ni mwanamazingira na anafafanua. "Limejitengeza kwa sababu ya mimea kutooza. Mwaka mzima dimbwi lina maji na liko chepechepe. Maji yakijaa mahali kasi ya mimea kuoza inapungua. Gesi za kaboni na methane huhifadhiwa humo ndani. Tulipo pana kina cha kilomita kumi. Tukilipoteza dimbwi gesi nyingi itatapakaa angani jambo litakaloleta athari kwa tabia ya nchi."

Mchango wa Ziwa Naivasha

Kulingana na wakaazi, dimbwi la Ondiri awali liliitwa Old Lake na mkoloni na kubadilishwa hadi jina lake la sasa. Unaporukaruka kwenye eneo hilo lisilokuwa na msingi, linatetema na unaweza kutumbukia. Inasadikika awali waliotumbukia walipatikana kwenye eneo la Ziwa Naivasha. Mzee David Kamau ana umri wa miaka 74 na ni mkulima wa mboga pembezoni mwa dimbwi la Ondiri na anakiri kuwa awali lilikuwa ziwa.

"Kutokea zamani hili eneo lilikuwa ziwa. Lakini Mungu aliwaonea wakazi huruma na kuruhusu nyasi kuota na kuwawezesha kuvuka kwa miguu maana walikuwa wanahangaika. Wanapita bila uoga japo dimbwi linatetema. Kulingana na wanavyosema maji haya yanatokea Naivasha na kuwa mtu akitumbukia humu atapatikana Ziwa Naivasha."
Ondiri ni chanzo cha mto Nairobi na nyasi maalum humea kila wakati bila ya kukauka katika misimu yote. Baadhi ya nyasi hizo huchukua muda mrefu kuoza na hicho hulifanya eneo la Ondiri kuwa na umuhimu mkubwa katika kuhifadhi gesi ya carbon. Hata hivyo miti ya kiasili imekatwa na aina nyengine inayohitaji maji mengi zaidi kupandwa hapo Ondiri. Ili kuwaelimisha wakazi kuhusu manufaa ya kuhifadhi dimbwi la Ondiri, vijana wanaojali mazingira wameanzisha harakati za kulinda eneo hilo.

Kenia Nairobi Ondiri Sumpf
Mahindi na mboga zilizopandwa pembezoni mwa Dimbwi la OndiriPicha: DW/Thelma Mwadzaya

Samuel Kinyanjui ni mwanachama wa kikundi cha Ecopro na anaelezea kuwa dimbwi hilo ni mazingira muhimu kwa viumbe vya majini na pia ni chanzo cha maji ya Mto Nairobi. "Watu wanaongezeka na mazingira kama haya yanafaa kutunzwa ila wakazi hawajui umuhimu wa Dimbwi hili kwani hawana elimu ya kutosha ya mazingira. Mifumo ya kilimo inaweza kubadilishwa na kuacha matumizi ya mbolea zilizo na kemikali ambazo kukinyesha zinaishia majini. Hilo linaathiri wanyama na ndege wa majini wanaoishi Ondiri."

Mabomba ya maji

Miti na mimea ya majini ndicho unachokiona ukiwasili kwenye dimbwi la Ondiri. Mabomba ya maji nayo pia yanang'ang'ania nafasi na miti ya eneo hilo. Maji hayo ni ya matumizi kwa wakazi wa Kikuyu. Baadhi ya kampuni hizo za maji zina vibali vya kufyonza maji. Kilimo pia kinahatarisha viumbe wa Ondiri kwa sababu ya kemikali za mbolea na dawa.

Kenia Nairobi Ondiri Sumpf
Barabara kuu ya kusini mwa Nairobi inayopita karibu na dimbwi la OndiriPicha: DW/Thelma Mwadzaya

Maureen Wambui ni mwanaharakati wa mazingira wa kikundi cha Ecopro huko Kikuyu na kwa mtazamo wake. "Miti ni muhimu na tunataka tuungane na wenzetu tupande miti ili tulinde mazingira. Miti hii iliyoko inashikilia mchanga na inaweza kukatwa kila baada ya miaka saba. Hizi nyasi za majini nazo zinatumiwa kulisha mifugo na pia kuezekea mapaa ya nyumba."

Makubaliano ya Ramsar kulinda maeneo chepechepe

Kwa sasa ni maeneo sita tu yenye kinamasi na maji yanayotambulika kimataifa kuwa muhimu. Maeneo hayo ni pamoja na Bonde la Mto Tana, maziwa ya eneo la bonde la ufa ya Bogoria, Naivasha, Elementaita. Maeneo hayo yanapatikana kwenye asiliamia kati ya 3 na 4 ya ardhi ambayo inaweza kuongezeka wakati wa msimu wa mvua.

Mwaka 1990 Kenya iliridhia makubaliano ya usimamizi wa maeneo yenye kinamasi yaliyo na umuhimu kimataifa. Kwa sasa kinachohitajika ni sheria muafaka za kuyalinda maeneo mengine yenye kinamasi kama vile dimbwi la Ondiri ambalo halijatambuliwa rasmi. Maeneo mengine ya kinamasi na maji ambayo si asili ni pamoja na mabwawa, vidimbwi vya maji, mashamba ya mpunga na vidimbwi vya kusafishia maji taka. Dimbwi la Ondiri lina mandhari ya kuvutia na baadhi hubarizi kwenye eneo hilo tulivu.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Mhariri: Josephat Charo