Congo: zawadi ya rais Tshisekedi kwa Wabunge yazuwa gumzo | Matukio ya Afrika | DW | 23.06.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Congo: zawadi ya rais Tshisekedi kwa Wabunge yazuwa gumzo

Zawadi ya gari iliyotolewa na Rais Tshisekedi kwa kila mbunge nchini Congo imezuwa gumzo , huku mgomo wa wahudumu wa afya ukiingia wiki yake ya pili. 

Zawadi ya gari iliyotolewa kwa kila mbunge nchini Congo na  Rais Felix Tshisekedi imezuwa gumzo nchini humo, huku mgomo wa waalimu na wahudumu wa afya wanaodai nyongeza za mishahara ukiingia wiki yake ya pili. 

Wabunge 500 wa bunge la Kongo kila mmoja mepewa gari kama zawadi na rais wa nchi hiyo. Shirika la uchunguzi wa matumizi ya fedha za umma nchini Congo,ODEP,  limesema zawadi ya rais Tshisekedi kwa wabunge ni rushwa.

Shirika hilo linatarajia kuwasilisha kesi mahakamani. Valerie Madianga msemaji wa shirika la ODEP amesema ni lazima viongozi kuwajibishwa.

''Hayo yamefanyika wakati ambapo hospitali hazina vitanda , hazina magodoro, waalimu manalipwa chini ya dola mia kwa mwezi.Wafanya kazi wa umma hawalipwi mishahara kwa miezi kadhaa sasa. Kwa kweli ni aibu kubwa sana.'',alisema Madianga.

''Fedha zimetoka wapi ?''

Mashirika ya kiraia na yale ya kutetea haki za binadamu pia yameunga mkono hatua ya kufanyika uchunguzi kuhusu fedha zilizotumiwa kununua magari hayo. Jean-Calude Katende, Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la ASADHO amesema wabunge wanapaswa kususia zawadi hiyo kwa maslahi ya wananchi.

'' Fedha hizo zimetoka wapi ? bajeti gani ilitenga fedha hizo ? tunapotizama bajeti ya mwaka 2021 hamna garama ya ununuzi wa gari kwa wabunge. Ikiwa hakuna bajeti ya ununuzi wa gari basi kuna kashfa ya rushwa. Ni sikitiko kubwa sana kwetu kwa sababu raia wamekumbwa na matatizo mengi '', alisema Katende.

Hayo yametokea huku wahudumu wa afya na waalimu kwenye baadhi ya shule wakiwa wako kwenye mgomo. Kwa miezi saba sasa wahudumu wa afya kwenye hospitali za umma hawalipwi mishahara yao.

Ukimya wa Ikulu ya rais

Jumamosi spika wa bunge Christophe Mboso alisikika akiwambia kwenye mkutano wa siri wabunge wa chama cha rais Tshisekedi kuwa rais ametoa zawadi ya gari la kifahari (SUV) aina ya Hyundai Palisade kwa kila mbunge. Kwa mujibu wa shirika la uchunguzi wa matumizi ya fedha za umma nchini Congo,ODEP ni kwamba gharama ya zawadi hiyo ni dola za marekani milioni 27.

Spika wa bunge alisema zawadi hiyo ni kufuatia hatua ya wabunge hao kukihama chama cha aliekuwa rais Joseph Kabila na kujiunga na ''Union Sacrée'' muungano mpya wa kisiasa wa rais Tshisekedi. Hadi sasa hakuna kauli yoyote ya rais Tshisekedi au ofisi yake kufuatia kashfa hiyo.