Chung Mong Joon kuwania urais wa FIFA | Michezo | DW | 17.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Chung Mong Joon kuwania urais wa FIFA

Aliyekuwa makamu wa rais wa FIFA Chung Mong Joon ametangaza rasmi nia yake ya kugombea uchaguzi wa rais wa Shirikisho hilo la Kandanda la Kimataifa

Akizungumza leo mjini Paris, Chung amesema rais ajaye lazima awe kiongozi wa kutatua migogoro na mwanamageuzi, kutokana na kashfa zilizoliandamana shirikisho hilo hivi karibuni. "Suala kuu katika uchaguzi ujao ni ikiwa mfumo wa miaka 40 wa rushwa unapaswa kuendelea au la. Mshirika huanza kuwa fisadi wakati kiongozi anadhani hawezi kufanywa chochote. Ikiwa nitachaguliwa, nitahudumu tu kwa muhula mmoja, miaka minne. Ninaweza kuibadilisha FIFA katika miaka minne: Hii ndio ahadi yangu kwa mashabiki wa kandanda ulimwenguni".

Chung, raia wa Korea Kusini mwenye umri wa miaka 63 atalenga kumrithi Sepp Blatter, ambaye alichaguliwa kuongoza kwa muhula wa tano mwezi Mei lakini akatangaza kujiuzulu kutokana na uchunguzi wa rushwa unaofanywa na Marekani na Uswisi katika shirikisho hilo.

Rais wa Shirikisho la Kandanda Ulaya – UEFA Michel Platini tayari alitangaza kugombea urais wa FIFA utakaofanywa katika mkutano maalum wa baraza kuu la FIFA Februari 26 mwaka ujao.

Chung ameahidi uwazi zaidi wa kifedha, akisema atafichua mshahara anaopata rais wa FIFA – kitu ambacho Blatter bado amekataa kukifanya. Mwanamfalme Ali bin Al Hussein wa Jordan, ambaye alishindwa na Blatter katika uchaguzi uliopita huenda akagombea tena. Nyota wa zamani wa Brazil Zico na rais wa shirikisho la kandanda la Liberia Musa Bility pia wanatathmini kujitosa katika kinyang'anyiro hicho.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga