1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Charles Taylor atiwa hatiani

Admin.WagnerD26 Aprili 2012

Aliyekuwa rais wa Liberia Charles Taylor amepatikana na hatia ya kutenda uhalifu wa kivita kwa kuyapa makundi ya waasi wa Sierra Leon silaha ili kujipatia almas za damu. Hukumu yake inatarajiwa kutolewa Mei 30 mwaka huu.

https://p.dw.com/p/14lHB
Charles Taylor akisikiliza maelezo ya kesi yake.
Charles Taylor akisikiliza maelezo ya kesi yake.Picha: picture-alliance/dpa

Hakimu aliyeongoza kesi hiyo Richard Lussick alimuambia Taylor kuwa ana hatia ya kusaidia katika uhalifu wote uliotendwa nchini Sierra Leon: "Mshatikiwa kwa matendo yake ana hatia yeye binafsi ya kusaidia kupanga, kutayarisha na kutenda uhalifu unaotajwa katika ibara za 3 na 4 za sheria kama ilivodaiwa katika mashtaka."

Hakimu Lussick aliongeza kuwa matendo ya Taylor alikuwa na ushawishi mkubwa katika uhalifu uliotendwa na alikuwa na dhamira ya kuchukua hatua ili kusaidia na kuunga mkono uhalifu. Baada ya kutolewa hukumu, Taylor atatumikia adhabu ya kifungo katika jela nchini Uingereza.

Taylor kama mmoja wa makatili wakubwa barani Afrika
Kama kiongozi wa waasi, mbabe wa kivita na baadae mkuu wa nchi, Taylor hakuwatesa tu raia wake nchini Liberia, bali pia aliwaunga mkono waasi wa Sierra Leon waliyofanya ukatili wa kutisha dhidi ya wananchi ikiwa ni pamoja na kuwakata mikono na vidole.

Katika kuunga mkono waasi wa Sierra Leon, lengo la Taylor lilikuwa kupata udhibiti wa migodi ya madini ya almas ya nchi hiyo jirani na Liberia na kuuza kile kilichokuja kuitwa almas za damu ili kuendesha vita vyake nchini Liberia vilivyochukua muda wa miaka 10 na kusababisha vifo vya watu laki moja na elfu 20.

Baadhi ya waathirika wa ukatili unaodaiwa kusababishwa na Taylor
Baadhi ya waathirika wa ukatili unaodaiwa kusababishwa na TaylorPicha: picture-alliance/dpa

Taylor alikuwa akiwapa silaha waasi wa Revolutionary United Front (RUF) na wao kumpatia almas hizo walizokuwa wanaziweka katika chupa ndogo na kumpelekea. Waasi hao waliauwa na kuwabaka raia wa Sierra Leon. Pia walikuwa wakikata viungo vyao kwa kutumia mapanga.

Maelfu ya watu nchini Sierra Leon walishangalia kwa vifijo baada ya kusikia kwamba Taylor amepatikana na hatia kwa kuhusika na vita vya kikatili katika nchi yao. Jusu Jarka, aliyekatwa mikono yote, alisema amefurahi kwamba mahakama ya nchini Uholanzi imebainisha kwamba Taylor binafsi alihusika na uhalifu waliotendewa watu wa Sierra Leon. Vita hivi viliisha mwaka 2002.

Baada ya kuaguka kwa utawala wake, Taylor alikimbilia nchini Nigeria ambapo Umoja wa Mataifa uliamuru akamatwe mwezi Juni mwaka 2003. Taylor alikuja kukamatwa Machi 2006 wakati akijaribu kuvuka mpaka kuelekea Cameroon na kukabidhiwa kwa Mahakama hiyo maalumi ya Umoja wa Mataifa ya Sierra Leon mjini Freetown.

Charles Taylor siku alipopelekwa kukabiliana na mkono wa sheria.
Charles Taylor siku alipopelekwa kukabiliana na mkono wa sheria.Picha: picture-alliance/dpa

Miaka mitano ya kesi na juhudi za kumhusisha Taylor na uhalifu huo
Kesi hii ilianza kusikilizwa mwezi Juni mwaka 2007 lakini kutokana na hofu ya kuyumbisha kanda hiyo kisiasa, iliamuliwa ihamishiwe mjini The Hague. Kesi hiyo imehusisha kuitwa kwa maafisa kadhaa wa ngazi za juu. Alpha Sesay, mwakilishi wa shirika la haki za binadamu la Open Society Justice Initiative aliyefuatilia kesi hii kwa niaba ya shirka lake anasema:

"Ingawa upande wa mashtaka ulitumia ushahidi wa maandishi, lakini ushahidi wake mkuu ulikuwa wa ndani - hapa namaanisha maafisa waliohudumia katika vyombo vya usalama wakati wa Taylor waliokuja na kutoa ushahidi dhidi yake - akiwemo makamu wake wa zamani."

Sesay anasema ingawa hakukuwa na ugumu katika kuthibitisha makosa yaliyofanwa na waasi wa Liberia, kazi kubwa ya upande wa mashtaka ilikuwa kuhusisha makosa hayo na Taylor.

"Hakuwahi kwenda Sierra Leon. Ushahidi ulikuwa kwamba baadhi ya makamanda wake na waasi wa Sierra Leon walikuwa wakienda Liberia na kurudi Sierra leon kuendesha operesheni hizo," anasema.

Ingawa mchakato huu mrefu wa kutafuta maandishi na mashahidi umekosolewa na baadhi ya watu, Profesa Harman van der Wilt, wa makosa ya kimataifa katika chuo kikuu cha Amsterdam anasema kesi za miaka zaidi ya mitatu ni za kawaida katika sheria ya kimataifa ya makosa ya jinai.

Moja wa mashahidi muhimu katika kesi hii, mwanamitindo maarufu Naomi Campbell
Moja wa mashahidi muhimu katika kesi hii, mwanamitindo maarufu Naomi CampbellPicha: AP

"Hata kwa kesi nyepesi kama ya Lubanga, ilichukua miaka. Hukumu ilitolewa mwezi Machi, na kesi hii iliendelea kwa miaka mitano au sita pia," anasema Profesa Wilt.

Makosa aliyoshtakiwa nayo Taylor
Katika kesi hii, Taylor alishtakiwa kwa makosa 11 yakiwemo ya mauaji, ubakaji, utumwa, matumizi ya watoto kama wanajeshi na makosa dhidi ya binadamu. Kesi hii imezingatia kipindi kati ya mwaka 1996 na 2003 na imehusisha makosa yaliyotendeka nchini Sierra Leon peke yake.

Taylor mwenye miaka 64, bado haja shtakiwa kwa makosa ya kivita nchini Liberia. Endapo atatiwa hatiani, Taylor anaweza kufungwa maisha katika gereza lililoko nchini Uingereza.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\Leslie Andre\DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman