1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League duru ya tatu yarejea viwanjani

Sekione Kitojo
16 Oktoba 2017

Champions League duru ya  tatu yarejea  tena  uwanjani , Borussia Dortmund yahitaji  ushindi dhidi  ya  APOEL Nikosia.

https://p.dw.com/p/2lvcA
Fußball Fussball, Champions League, Manchester City vs Shakhtar Donetsk
Kocha wa Manchester City Pep GuardiolaPicha: picture-alliance/Citypress 24/D. Chesterton

Katika  Champions League  barani  Ulaya  kesho vumbi  litatimka pale miamba  wa Manchester City  watakapokabana koo  na  Napoli ya  Italia  katika  kundi F kesho  Jumanne. Viongozi  hao  wa Premier League  na  Serie A  wamekuwa  wakitamba  katika  ligi  zao wakifunga  mabao  wapendavyo.

Mara  ya  mwisho  timu  hizo kushindwa  kupata  ushindi  katika  ligi  zao  ni  wakati  City ilipotoka sare  na  Everton mwezi  Agosti.

Katika michuano  ya Ulaya , ni City  ambayo  ina rekodi nzuri  kwa kuishinda  Feyernood ya  Uholanzi  na  Shakhtar Donetsk, wakati Napoli ilishindwa ilipokutana  na  mabingwa  hao  wa  Ukraine. Kwa hiyo klabu  hiyo  kutoka  Italia  itakuwa  katika  mbinyo  wa kupata matokeo  mazuri  wakati  watakapokwenda  mjini  Manchester kupambana  na  City  katika  uwanja  wa  Etihad.

Msisimko  mwingine  uko  katika  kundi  H  ambapo  mabingwa watetezi misimu miwili  Real Madrid watakapokuwa  wenyeji  wa Tottenham Hot Spurs kesho  Jumanne. Madrid  na  Tottenham wameshinda  mara  mbili  kila  mmoja na  kuziweka  Borussia Dortmund  na  APOEL Nikosia  katika  hali  ya mashaka  makubwa kuweza  kufuzu  kuingia  katika  timu 16  bora. Dortmund  inasafiri kwenda  Nikosia kupambana  na  APOEL  timu  zote  zikiwa  hazina pointi.

Fußball Champions League Borussia Dortmund v Real Madrid Torjubel Aubameyang
Mshambuliaji wa Borussia Dortmund Pierre-Emerick AubameyangPicha: Reuters/W. Rattay

Mkurugenzi wa  sporti  wa  Borussia Dortmund Michael Zorc amesema ushindi  ni  muhimu  ili  kufufua  matumaini  yao  ya  kuingia katika  awamu  ya  mtoano  ya  timu  16 zitakazosalia. Kikosi  cha kocha Peter Bosz kilipata  kipigo  cha  kwanza  nyumbani  baada  ya michezo 41 katika  Bundesliga  Jumamosi dhidi  ya  Leipzig  ambayo nayo  sasa  inalenga  kupata  ushindi  wake  wa  kwanza  katika mashindano  ya  Ulaya  wakati  itakapokuwa  wenyeji  wa  Porto  ya Ureno  katika  kundi G kesho  Jumanne.

Sevilla inaweza  kubakia  kiongozi  wa  kundi  E itakapozuru Spartak Moscow kesho. Sevilla ina  pointi  nne, mbili  zaidi ya  Spartak  na Liverpool.

Champions League - Paris St Germain vs Bayern München Neymar Mbappe Cavani
Washambuliaji hatari wa PSG , Neymar, Mbappe na CavaniPicha: Getty Images/AFP/C. Simon

Kudhibiti kimbunga  cha  mashambulizi cha  Paris Saint Germain  cha kina  Neymar, Kylian Mbappe na  Edinson Cavani  ni  mtihani mkubwa  kwa  safu  ya  ulinzi  ya  Anderlecht  ya Ubelgiji  siku  ya Jumatano. Na  PSG inaelekea  kupata  ushindi  wake  wa  tatu katika  kundi  B.

Katika  kundi  hilo  la  B kuna  pia  Bayern Munich ambayo inakwaana  na  Celtic siku  ya  Jumatano, ikiwa  chini  ya  kocha mpya Jupp Heynckes  aliyeshawishiwa  na  viongozi  wa  Bayern kusitisha  muda  wake  wa  kustaafu na  kuja  kukinoa  kikosi  hicho.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae / ape

Mhariri: Mohammed  Abdul-Rahman