Catalonia huenda ikajitangazia uhuru wake | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Catalonia huenda ikajitangazia uhuru wake

Kiongozi wa Catalonia anatarajiwa kuwahutubia wabunge wa mkoa huo hii leo katika hotuba ambayo wafuasi wake wana matumaini kwamba itakuwa ni tamko la kutangaza uhuru wa jimbo hilo.

Wakati hotuba hiyo ikisubiriwa, kiongozi huyo ameendelea kupata shinikizo kutoka ndani na nje ya nchi akitakiwa kusitisha mpango huo. Hotuba hiyo anayotarajiwa kuitoa katika bungeni la jimbo la Catalonia, kiongozi wa jimbo hilo Carles Puigdemont, imeibua wasiwasi wa usalama katika Umoja wa Ulaya.

Viongozi wa kisiasa wamewatolea mwito Wacatalonia wanaotaka kujitenga kusitisha mpango wao huo na kuinusuru Uhispania na mgogoro mbaya zaidi katika miongo kadhaa iliyopita. Meya maarufu wa mji wa Barcelona Ada Colau amepinga azma ya Catalonia kujitangazia uhuru. "Oktoba mosi imefungua milango ya majadiliano. Imeiweka Catalonia katika ramani. Mataifa mengi na taasisi za kimataifa zinaunga mkono majadiliano. Lakini pia wanaonya wazi kwamba hawatakuwa nyuma yenu ikiwa mnashikilia uamuzi wa upande mmoja. Katika muktadha wa sasa kura ya maoni ya oktoba mosi haiwezi kuwa sababu ya kujitangazia uhuru. Lakini inaweka uwezekano wa kuanzisha majadiliano na usuluhishi wa kimataifa," amesema Colau.

Spanien Referendum Katalonien (picture-alliance/Zumapress/M. Oesterle)

Raia wa Catalonia wakisubiri kupiga kura Oktoba mosi

Kiongozi wa upinzani cha Kisoshalisti nchini Uhispania pia ameungana na serikali kupinga uhuru wa jimbo la Catalonia. Lakini pia upinzani umetoka nje ya nchi.Waziri wa Ufaransa anayehusika na masuala ya Umoja wa Ulaya Nathalie Loiseaualisema ikiwa Wacatalonia watajitangazia uhuru basi utakuwa wa upande mmoja na kutotambulika kimataifa. 

Kwa upande mwingine,  chama kinachoongoza Scotland, Scottish National Party kimeunga mkono hatua hiyo na kusema serikali ya Uhispania inapaswa kuheshimu matokeo ya "Ndiyo" ya kura ya maoni iliyofanyika Oktoba mosi licha ya kupigwa marufuku na Madrid, ambapo asilimia 43 ya wapiga kura walijitokeza.

Puigdemont amesema kura hiyo ilidhihirisha watu wanataka kujitenga na wafuasi wake wanamtaka atangaze uhuru suala ambalo ni kwenda kinyume na serikali kuu na mahakama za kitaifa.

Spanien Regierungssprecherin Vizepräsidentin Soraya Saenz de Santamaria (dapd)

Naibu waziri mkuu wa Uhispania Soraya Saenz de Santamaria

Naibu waziri mkuu wa Uhispania Soraya Saenz de Santamaria ameonya jana kwamba hatua ya kujitangazia uhuru haitaachwa hivi hivi ."Ninachoweza kusema kama watajitangazia uhuru wa upande mmoja hautakuwa na athari. Ni wajibu wa serikali ya Uhispania kupitia seneti, kwasababu nataka kukumbuka kwamba huu ni mchakato wa kisheria, wa kuchukua hatua".

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker wamezungumza na waziri mkuu Mariano Rajoy kwa njia ya simu mwishoni mwa juma. Merkel amesema anaunga mkono umoja wa Uhispania na wote walibadilishana mawazo namna gani mazungumzo ya ndani ya Uhispania yanavyoweza kutekelezwa katika kwa kuheshimu misingi ya katiba.

Utafiti wa maoni uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kwamba wacatalonia wamegawanyika kuhusu suala la kujipatia uhuru, ingawa viongozi wa mkoa wanasema vurugu za polisi wakati wa kura ya maoni zimechangia wengi kutofautiana na serikali kuu mjini Madrid.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com