1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yamtuhumu kiongozi wa upinzani kwa 'ugaidi'

Tatu Karema
23 Septemba 2021

Burundi yamtuhumu kiongozi wa upinzani kwa 'ugaidi'

https://p.dw.com/p/40knp
Burundi Opppositionspolitiker Alexis Sinduhije
Picha: Getty Images/AFP/E. Ndikumana

 

Tangazo hilo la Nyandwi lililotolewa jana jioni limefuatia mfululizo wa mashambulizi katika siku za hivi karibuni katika taifa hilo la Afrika ya Mashariki yaliosababisha vifo vya watu sita na kujeruhiwa kwa mamia ya wengine. Nyandwi ameongeza kuwa waranti huo unahusisha mashambulio ya awali yanayojumuisha milipuko ya guruneti na uvamizi ambao ulisababisha vifo vya mamia ya watu na kujeruhiwa kwa wengine wengi tangu mwanzoni mwa mwaka 2020.

Pia amedai kuwa uchunguzi ambao tayari umefanywa umefichua kuwa maovu hayo yanafanywa na kundi la kigaidi linaloongozwa na Sinduhije. Nyandwi amesema kuwa chini ya sheria za kitaifa na kimataifa, vitendo hivyo vinachukuliwa kuwa vya ugaidi, na pia uhalifu dhidi ya binadamu. Sinduhije ambaye ni rais wa vuguvugu la upinzani la Movement for Solidarity and Development MSD, kwa muda mrefu amekuwa akishukiwa na serikali ya Burundi kuwa katika uongozi wa kundi la waasi la RED-Tabara nchini humo madai ambayo amekuwa akikana kila wakati.

Tuhuma dhidi ya kundi la RED-Tabara

Kundi hilo liliibuka miaka 10 iliyopita na linatuhumiwa kwa kuhusika katika mashambulio mabaya ama uvamizi nchini Burundi tangu mwaka 2015. Mnamo mwaka 2020, kundi hilo lilisema kuwa lilihusika katika mfululizo wa mashambulio yaliosababisha vifo vya zaidi ya watu 40 kutoka kwa vikosi vya usalama na tawi la vijana la chama tawala cha  CNDD-FDD.

Mashambulio mabaya pia yalifanyika katika mji mkuu Gitega siku ya Jumapili jioni na Bujumbura Jumatatu jioni. Kundi hilo bado halijatoa tamko kuhusiana na mashambulio hayo. Hata hivyo, mwanasheria huyo mkuu amesema kuwa milipuko hiyo ilihusishwa na mashambulio ya awali ambapo Sinduhije anashtakiwa kufanya. Hakutoa maelezo zaidi na madai hayo pia hayakuweza kuthibitishwa.

Siku ya Alhamisi, kundi la MSD lilikataa kile lililosema ni tuhuma zisizo na msingi za serikali isiyo na uwezo wa kuhakikisha usalama wa raia wake. Waranti pia umetolewa dhidi ya Francois Nyamoya, katibu mkuu wa kundi hilo la MSD anayeishi nchini Rwanda na Marguerite Brankitse, mwanzilishi wa nyumba ya watoto mayatima ya Maison Shalom anayeishi nchini Rwanda na Ulaya. Nyandwi amesema kuwa wanaziomba nchi hizo wanamoishi washukiwa hao kushirikiana na serikali ya Burundi kuwakamata ili kuepusha mauaji zaidi ya raia wa nchi hiyo.