1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaThailand

Bunge la Thailand lavunjwa kwa ajili ya uchaguzi mpya

12 Desemba 2025

Waziri Mkuu wa Thailand Anutin Charnvirakul amelivunja bunge leo Ijumaa ili kujiandaa kwa uchaguzi mpya mapema mwakani, wakati taifa hilo likiwa katikati ya mapigano na Cambodia.

https://p.dw.com/p/55E0L
Thailand Bangkok 2025 | Anutin Charnvirakul baada ya mkutano wa Baraza la Usalama wa Kitaifa - NSC kuhusu mgogoro wa Cambodia
Waziri Mkuu wa Thailand Anutin Charnvirakul baada ya kuongoza mkutano wa Baraza la Usalama wa Kitaifa (NSC) katika Ikulu ya Serikali huko Bangkok mnamo Novemba 11, 2025. Picha: Chanakarn Laosarakham/AFP/Getty Images

Waziri Mkuu Anutin aliyedumu madarakani kwa takribani miezi minne, amelivunja Baraza la Wawakilishi baada ya kupewa idhini na Mfalme Maha Vajiralongkorn.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari mapema leo mjini Bangkok, Anutin alisema uamuzi huo ulitokana  na hatua ya chama kikuu cha upinzani cha People kuondoa uungaji wake mkono bungeni.

Ni hatua inayochukuliwa huku kukiwa na kipindi kigumu cha kisiasa, kinachoshuhudia mapigano makali kati ya Thailand na Cambodia ambapo maelfu ya watu pande zote mbili za mpaka wanayakimbia makaazi yao.