Bunge la Misri kuidhinisha mageuzi ya katiba | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.04.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Wabunge wengi wa Misri wanamuunga mkono El Sisi

Bunge la Misri kuidhinisha mageuzi ya katiba

Mageuzi yanayopitishwa yatafungua njia ya kumruhusu rais El Sisi kubakia madarakani mpaka 2024 muhula wake utakapofikia mwisho na hata kuitawala nchi hiyo mpaka 2030

Magauezi ya katiba yanayofanywa na bunge la Misri yatatowa nafasi ya kuongezwa muhula wa sasa wa rais Al sisi kutoka miaka minne mpaka miaka 6 na hivyo kumfanya abakie madarakani mpaka mwaka 2024.Kipengee kingine kinachofanyiwa marekebisho maalum kinahusu kumruhusu al Sisi  agombee tena muhula wa tatu madarakani na kumpa uwezekano wa kuendelea kuiongoza Misri mpaka mwaka 2030.

Mabadiliko hayo yanamruhusu rais kuwateua watakaochukua nyadhifa za juu za mahakama sambamba na kubeba dhima kubwa ya jeshi la nchi. Mabadiliko hayo yanabidi yaidhinishwe na alau thuluthi mbili ya bunge la Misri lenye wajumbe 596 kwa ujumla kabla hayajapelekwa kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni. Kimsingi bunge la Misri hivi sasa linahodhiwa na wanaomtii moja kwa moja al Sisi.

Na kinachosikika kwenye ndimi za wengi wanaomuunga mkono rais huyo wanasema mageuzi hayo ni muhimu kwa ajili ya uthabiti wa muda mrefu na wakudumu katika Misri wakati wapinzani kwa upande wa pili wakisema mageuzi haya yanalenga kumuongezea nguvu rais sisi kuendelea kushikilia madaraka na kukiuka uhuru wa mfumo wa mahakama na sheria.

Al sisi aliingia madarakani mwaka 2014 mwaka mmoja baada ya kuongoza harakati za kumuondowa madarakani rais aliyechaguliwa kihalali katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia Mohammed al Mursi,kufuatia maandamano makubwa ya umma dhidi ya utawala wake. Mwaka jana al sisi alichaguliwa kurudi madarakani kwa kishindo katika uchaguzi uliompambanisha yeye na mgombea mmoja tu aliyejitangaza kuwa mtiifu kwake.

Kinachoendelea leo hii katika bunge la Misri kwa sasa ni majadiliano ya mwisho juu ya mageuzi hayo ya katiba ambayo kwa jicho la wapinzani wanayaita kuwa ni hatua moja inayoirudisha nyuma Misri katika utawala kamili wa kiimla. Pindi mageuzi hayo yanapitishwa,wananchi watahitajika kujiandaa kuingia katika mchakato wa kuyapigia kura ya maoni mwanzoni mwa mwezi ujao wa Mei  wakati zitakapokuwa zimeanza ibada za funga ya  mwenzi mtukufu wa Ramadhani kwa waislamu wote duniani.

Ikumbukwe kwamba tangu mwezi Aprili mji mkuu wa Misri,Cairo umekuwa ukibandikwa picha na mabango makubwa yenye ujumbe wa kuwahimiza wananchi kushiriki katika kura ya maoni kuunga mkono mageuzi hayo ya katiba. Harakati hizo za kuweka mabango na picha zinaelekea kufadhiliwa na vyama vinavyoiunga mkono serikali,wafanyabiashara na wabunge.

Kimsingi rais al Sisi anatakiwa kumaliza muda wake madarakani mwaka 2022 lakini kutokana na mageuzi hayo yanayopigiwa upatu hapana shaka Misri itaendelea kutawaliwa na kiongozi huyo wa kijeshi,na sababu hakuna sababu yoyote iliyotangazwa hadi sasa ya kwanini yanafanyika mageuzi hayo ambayo bila shaka yamefanywa na kamati maalum iliyoandaa muswaada wa mwisho wa sheria hiyo ya katiba.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Sekione Kitojo