1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram iliwaagiza wahalifu kuwateka wanafunzi

Sylvia Mwehozi
17 Desemba 2020

Maafisa wa usalama na viongozi katika jimbo la Katsina nchini Nigeria wameeleza kuwa, kundi la Boko Haram liliyaagiza makundi matatu ya kihalifu kuwateka nyara mamia ya wanafunzi wa kiume kwa niaba yao. 

https://p.dw.com/p/3mqc5
Nigeria Kankara | Angriff auf Schule | Entführte Schulkinder
Picha: Afolabi Sotunde/REUTERS

Kundi hilo la Boko Haram limedai kuhusika na shambulizi la Ijumaa, ambalo liliilenga shule ya sekondari katika mji wa Kankara jimboni Katsina. Lakini vyanzo tofauti katika eneo hilo vimelieleza shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba uvamizi huo ulifanywa na kiongozi wa genge moja anayeitwa Awwalun Daudawa aliyepewa maagizo na Boko Haram. Kiongozi huyo alishirikiana na viongozi wengine wawili wa magenge ya kihalifu.

Magenge hayo ya kihalifu, yameleta hofu katika jamii za maeneo ya Kaskazini magharibi mwa Nigeria kwa miaka mingi. Wataalamu walionya hivi karibuni juu ya jaribio la wanajihadi kuunda ushirika na makundi ya kihalifu. Afisa mmoja wa Usalama aliyezungumza na AFP amemuelezea Daudawa kama ''mnyang'anyi na mwizi wa ng'ombe kabla ya kuanza kutumia bunduki, akichukua silaha kutoka Libya ambako alipatiwa mafunzo na kuziuza kwa majambazi''.

Afisa huyo anaendelea kusimulia kwamba baada ya muda, kiongozi huyo alianzisha ushirika na Boko Haram akichukua silaha ambazo huchukuliwa kutoka mikononi mwa maafisa wa usalama wa Nigeria. Chanzo kingine ambacho kina uelewa na shughuli za ''majambazi" katika majimbo ya Katsina na Zamfara, kilieleza kwamba kulingana na taarifa zilizopo, Daudawa alipatiwa maagizo na kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau kuwateka wanafunzi wa kiume.

Nigeria Kankara | Angriff auf Schule | Entführte Schulkinder
Wazazi wa wavulana waliotekwa KatsinaPicha: Afolabi Sotunde/REUTERS

Baada ya wanafunzi hao kuchukuliwa, walienda karibu na mpaka na jimbo la Zamfara na kugawanyika katika makundi tofauti ya kihalifu kwa ajili ya kuwatunza wanafunzi, huku baadhi ya makundi yakifanya mawasiliano na mamlaka kwa ajili ya kuachiliwa. Taarifa hizo zilithibitishwa na gavana wa Katsina Aminu Bello Masari siku ya Jumatatu aliyeandika kupitia Twitter kwamba watekaji wamefanya mawasiliano na serikali.Lifahamu kundi la Boko Haram

Shambulizi hilo lilitokea mbali na ngome ya Boko Haram, eneo la Kaskazini mashariki ambako kundi hilo lilianzisha uaasi muongo mmoja uliopita. Wanajihadi hao walidai kuhusika na utekaji wa Ijumaa kupitia sauti ya dakika nne iliyotumwa kwa AFP. "Ninaitwa Abubakar Shekau na kaka zetu wamehusika na utekaji nyara huko Katsina'', ndivyo ilivyosikika sauti ya Shekau. Mmoja wa vijana aliyefanikiwa kutoroka Usama Aminu anaeleza waliyopitia.''Tulitembea usiku mzima msituni na kulipokucha walipata mahali na kutueleza tuketi chini. Wakati majambazi yaliposikia sauti ya helikopita angani wakatuambia tulale chini ya miti mikubwa na nyuso zikiwa ardhini.''

Shekau ndiye aliyehusika na utekaji nyara wa mwaka 2014 wa wasichana 276 wa shule ya Chibok. Utekaji huo ulichochea hasira, lakini chanzo kingine kinasema matukio hayo mawili siyo ya kulinganishwa. "Yapo makubaliano ya amani yanayoendelea baina ya magenge ya kihalifu na serikali ya jimbo la Zamfara ambayo majambazi hawataki kuyakiuka. Wamekuwa chini ya shinikizo kubwa kuwaachia wavulana", kilisema chanzo hicho. Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya zote zimetoa wito wa kuachiliwa wavulana hao ambao idadi yao bado haijakuwa wazi wengine wakisema ni kati ya 320 na 333 lakini waakazi wa Kankara wanasema ni zaidi ya 500.