1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden kutoa hotuba ya hali ya taifa

Bruce Amani
7 Februari 2023

Rais Joe Biden wa Marekani atatoa hotuba ya hali ya taifa miezi mitatu baada ya Warepublican kuchukua udhibiti wa Baraza la Wawakilishi. Hotuba ya Biden huenda ikawa ndio mwanzo wa msimu wa kampeni za urais wa 2024

https://p.dw.com/p/4NC7j
USA Präsident Joe Biden Rede zur Lage der Nation
Picha: Victoria Spartz/Getty Images

Biden atakuwa na fursa ya kueleza zaidi juu ya mitazamo ya umma kuhusu ukomo wa madeni, matumizi ya kijamii, vita vya Urusi nchini Ukraine na mada nyingine wakati akipanga kutangaza kampeni yake ya kuchaguliwa tena, katika wiki chache zijazo.

Pia inampa fursa ya kuimarisha uungwaji mkono miongoni mwa Wademocrat, baadhi ambao wana wasiwasi kuhusu umri wake na masuala mengine. Biden alifikisha umri wa miaka 80 Novemba, na kama atachaguliwa tena atakuwa na umri wa miaka 82 wakati anaanza muhula wa pili.

Nini Biden anatarajiwa kusema?

Biden anatarajiwa kutumia hotuba yake kama mwanzo usio rasmi wa msimu wa kampeni ya urais mwaka wa 2024, akitangaza sera za kipaumbele ambazo huenda zikapata au kutopata uungwaji mkono Bungeni.

Anatarajiwa kupigia debe mafanikio ya kiuchumi kufuatia mdoororo uliosababishwa na janga la UVIKO-19, kufanya ulinganisho mkubwa na vipaumbele vya baadhi ya wapinzani kutoka Republican na kutangaza ajenda za umoja ambazo anaamini zinapaswa kuvileta Pamoja vyama viwili vikuu.

USA Präsident Joe Biden Rede zur Lage der Nation
Biden atahutubia kikao cha pamoja cha bungePicha: Win McNamee/Getty Images

Hotuba hiyo imekuwa ikitengenezwa kwa wiki kadhaa na huhusisha rasimu nyingi kati ya Biden, waandishi wake wa hotuba na maafisa kadhaa wa kisiasa na sera katika serikali yake.

Mwaka jana, hotuba ya Biden ilijiri siku chache tu baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na iliangazia pakubwa kufafanua jibu la Marekani.

Nani anahudhuria?

Hotuba hiyo hutolewa wakati wa kikao cha Pamoja cha bunge. Wajumbe wote wa Baraza la Seneti linalodhibitiwa na Wademocrat na Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na Warepublican hualikwa. Mawaziri wa serikali ya Biden, wakuu wa jeshi, na Mahakama ya Juu pia huhudhuria.

Biden alialikwa rasmi kutoa hotuba ya hali ya taifa mwezi Januari na spika wa Bunge Kevin McCarthy. McCarthy ataongoza hafla ya leo na kuandamana na Makamu wa Rais Kamala Harris, ambaye pia ni rais wa Seneti.

Mtu mmoja ambaye hahudhurii ni Waziri mmoja wa serikali ya Biden ambaye atachaguliwa kuwa mtu aliyetengwa kwa ajili ya kuchukua uongozi wa nchi. Mtu huyo atawekwa katika eneo salama na anapewa jukumu la kuchukua usukani wa serikali kama patatokea mkasa utakaomdhuru rais na warithi wake wengine katika majengo ya Capitol.

Warepublican wamemchagua Gavana wa Arkansas Sarah Huckabee Sanders, aliyehudumu kama msemaji wa White House chini ya Donald Trump, kutoa jibu kwa niaba ya chama chao.

Reuters