1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden kuchunguzwa baada ya kukutwa na nyaraka za siri

Lilian Mtono
13 Januari 2023

Mwanasheria mkuu wa serikali nchini Marekani Merrick Garland amemteua mchunguzi maalumu Robert Hur kuchunguza tukio la kupatikana kwa nyaraka za siri katika makazi ya rais Joe Biden yaliyoko Wilmington, Delaware.

https://p.dw.com/p/4M6gm
USA Jahrestag des Aufstands im Kapitol | Präsident Joe Biden
Picha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Aidha mchunguzi huyoi atachunguza tukio la awali la kukutwa kwa nyaraka kama hizo za siri katika ofisi ya rais Joe Biden isiyokuwa na ulinzi iliyoko mjini Washington. Nyaraka hizo zinasadikika zilikuwepo kwenye ofisi hiyo tangu Biden alipokuwa makamu wa rais.

Katika tukio la kwanza, nyaraka hizo za siri zilipatikana wiki moja kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa mwaka uliopita, ambalo liliripotiwa na ikulu ya White House Jumatatu hii, hatua iliyoibua shutuma kutoka chama cha Republican, wakihoji sababu za kufichwa kwa taarifa hizo.

Kwenye ufichuzi huu wa karibuni, nyaraka hizo zimepatikana kwenye gereji ya nyumbani kwa Biden mjini Wilmington, Delaware, ambako mara nyingi huwa anakwenda kupumzika mwishoni mwa wiki, hii ikiwa ni kulingana na ikulu ya White House.

Mwanasheria huyo mkuu Garland amemteua Hur ambaye atachunguza iwapo kuwapo kwa nyaraka hizo kwenye makazi binafsi kunaweza kuwa kumekiuka utaratibu wowote wa kisheria. Garland anayeongoza wizara ya sheria, amesema anaamini kwa dhati kwamba mchakato huo wa kawaida unaoendeshwa na wizara yake utaifanya kazi hiyo kwa uadilifu.

Uteuzi wa Hur unafanyika masaa kadhaa baada ya White House kuripoti tukio hilo la pili la kupatikana nyaraka hizo za siri ingawa haikuelezea yaliyomo kwenye nyaraka hizo, hatua iliyoichochea kashfa ya awali iliyofichwa.

USA | Trump will bei Wahl 2024 erneut antreten
Rais wa zamani wa Marekani Dobnald Trump pia alikutwa na nyaraka za siri katika makazi yake ya Mar-a-Lago mwaka uliopita.Picha: Octavio Jones/REUTERS

Ikumbukwe mwaka uliopita maafisa wa shirika la upelelezi la ndani, FBI walifichua nyaraka 11,000 za siri kwenye makazi ya mtangulizi wa Biden, Donald Trump yaliyoko Mar-a-Lago Florida. Pamoja na tuhuma kuhusu nyaraka hizo, Trump pia anakabiliwa  na tuhuma za kuzuia juhudi za serikali za kuzipata nyaraka hizo.

Biden amewaambia waandishi wa habari kwamba anazichukulia kwa umakini mkubwa nyaraka hizo za siri na kusema wanashirikiana kikamilifu na maafisa wa wizara ya sheria katika uchunguzi huo.

"Lakini kama nilivyosema mwanzoni mwa wiki hii, watu wanajua ninazichukulia nyaraka hizi kwa umakini mkubwa. Pia nilisema tunashirikiana kikamilifu na wizara ya sheria. Mawakili wangu walipitia maeneo mengine kulikohifadhiwa nyaraka wakati nikiwa makamu wa rais. Na walimaliza kuyakagua jana usiku. Waligundua nyaraka chache zilizokuwa na muhuri wa siri kwenye makabati ya kuhifadhi mafaili nyumbani kwangu na kwenye maktaba yangu binafsi," alisema Biden.

Biden aidha, amewaambia waandishi wa habari akiwa Mexico City kwamba hakujua chochote kuhusiana na kupatikana kwa nyaraka kama hizo kwa mara ya kwanza November 2 mwaka jana.

Sprecherin Karine Jean-Pierre
Msemaji wa ikulu ya White House Karine Jean Pierre alijikuta katika wakati mgumu alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusiana na nyaraka hizoPicha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Wanasiasa wa chama cha Republican wameendelea kujitokeza kukosoa ufichuzi huu, baada ya spika wa bunge Kevin McCarthy kuungana na wawakilishi wenzake kushinikiza uchunguzi wa bunge, alipozungumza na waandishi wa habari huku akikumbushia namna Biden alivyomkosoa Trump baada ya tukio kama hilo.      

Soma Zaidi: Trump aruhusu kutolewa kwa nyaraka za siri za FBI

Hur aliyewahi kuteuliwa na Trump kuwa mwanasheria wa serikali katika huko Maryland ameahidi kufanya uchunguzi wa haraka, wa haki, usio na upendeleo wala huruma.

Msemaji wa ikulu ya White House Karine Jean Pierre alijikuta katika wakati mgumu alipokutana na waandishi wa habari waliotaka taarifa zaidi kuhusiana na ufuchuzi huo, ingawa alisisitiza tu kwamba rais Biden anazizingatia nyaraka hizo kwa umakini mkubwa na wasaidizi wake waliiarifui mara moja idara ya kumbukumbu ya wizara ya sheria. 

Wakili wa Biden, Richard Sauber amesema ana imani kwamba baada ya ukaguzi huo itathibitika kwamba nyaraka hizo ziliwekwa mahali hapo kimakosa.  

Soma Zaidi: Uchaguzi Marekni: Urusi haimtaki Biden, China yampinga Trump