Biashara yanawiri Libya | Masuala ya Jamii | DW | 12.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Biashara yanawiri Libya

Kutokana na kuondokana na vikwazo wananchi wa Libya wamekuwa wakikimbilia madukani, bidhaa ambazo kwa muda mrefu zimekuwa hazipatikani nchini humo sasa zimejaa chekwa chekwa wakati wimbi la mageuzi ya kiuchumi ya kutegemea msingi wa masoko na fedha za petroli vikichanganywa pamoja vimewafanya wale wenye akiba ya kutosha kuwa watumiaji waliokubuhu.

Hii ndio Libya ya sasa.

Hii ndio Libya ya sasa.

Magari yanayongara barabarani na pikipiki za mwendo wa kasi yanatamba katika mitaaa ya mji mkuu wa Tripoli ambao wakati fulani ilikuwa imelala na sasa imekuwa maskani ya mahoteli kadhaa mapya ya kibinafsi na maduka makubwa makubwa ya bidhaa.

Katika mtaa wa Gergaresh wataalamu na wale wenye nacho au wenye kujiweza hujimwaga kwenye maduka ya nguo kutumbuwa kwa matumizi ya mavazi ambapo suruali aina ya jeans huwagharimu dola 80 machine ya kufanyia mazoezi dola 1,300 na chupa za mafuta mazuri dola 250.

Mfumuko huo wa kutumbuwa umechochewa na kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya nchi hiyo kufuatia maamuzi yake makuu mawili muhimu hapo mwaka 2003 ambapo taifa hilo la Afrika Kaskazini liliachana na harakati za kutengeneza silaha za maangamizi na kukubali kuwajibika kwa raia wake kuhusika na uripuaji wa ndege ya shirika la ndege la Marekani katika anga ya Lockerbie Scotland hapo mwaka 1988 ambapo watu 270 waliuwawa.

Mageuzi yenye nia ya kuutanuwa uchumi kutoka mafuta na kuimarisha makampuni ya kibinafsi kwa kiasi kikubwa yamewanufaisha matajiri katika nchi hiyo mwanachama wa shirika la nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani OPEC yenye idadi ya watu milioni 6.

Lakini hata hivyo Walibya walio maskini wana nafasi mbali mbali za kuchaguwa bidhaa za chakula na zile za matumizi ya nyumbani kuliko ilivyokuwa miaka mitano iliopita ambayo ni mabadiliko yanayokaribishwa na watu ambao wanakumbuka wazi wazi uhaba wa mahitaji muhimu katika miaka ya 1980.Makampuni binafsi wakati huo yalikuwa yamepigwa marufuku nchini Libya.

Lakini Walibya wanasema utajiri wa kifedhuli bado ungali unachukiwa na kwamba bidhaa rahisi za umeme za China na zile za anasa za bei ya wastani kama vile chokoleti na chizi zimekuwa zikifurahiwa.

Nyingi ya fedha zinazotumika madukani na katika uwekezaji wa mali hutoka kwa Walibya wenye ushawishi wa kisiasa ambao wamefanikiwa kuanzisha biashara za mafanikio kwa kutumia uhusiano wao na serikali.

Walibya wengine bado hawakujiunga na kunawiri huko kwa matumizi au kutumbuwa na lazima wafanye kazi mbili au tatu ili kuweza kuwa na akiba.

Mwananchi mmoja mwenye duka dogo ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema matajiri wanafurahia maisha mazuri wakati wengi wao wanaishi kwa kujikimu tu.

Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi anaungalia mwenendo huo wa uchu kwa makini na hapendelei yale yote anayoyaona,kwake yeye kunawirika kwa biashara ya reja reja ni kitengo tu cha uchumi unaotanuka unaotegemea mafuta.

Hapo mwaka jana amekaririwa akisema kwamba watu wanadanganyika na mishahara ya petroli kufuatia ziara yake katika mji wa Sheba ambao umenawiri kwa maduka, masoko na mikahawa kwamba kila kitu kinachozalishwa duniani kinapatikana hapo.

Gaddafi aliuliza nani anayenunuwa bidhaa hizo?Na kujijibu mwenyewe kwamba ni watu wenye mishahara kutoka Benki Kuu ,Hazina au kutoka Petroli. Amekuita kunawiri huko kwa maisha kuwa ni bandia.

Anataka biashara za reja reja ziwekeze katika viwanda ambavyo hutowa ajira ya kudumu kwa kutengeneza vitu ambavyo watu wanataka kununuwa.

Wafanyabiashara wenye kupendelea mageuzi na washauri wa Gaddafi juu ya uchumi wa nchi za magharibi wanakubaliana na dira yake lakini wanasema wawekezaji kwanza wanataka kuhakikishiwa kwamba mageuzi ya kiuchumi ya kutegemea nguvu za soko yanabakia nchini humo.

Libya ambayo hujipatia zaidi ya dola bilioni 30 kwa mwaka kutokana na mafuta imetenga dola bilioni 19 kwa ajili ya miradi ya ujenzi kwa mwaka 2007 na kuamsha ushindani wa kuwania zabuni kwa makampuni ya kigeni.

Abdulla Fellah mwenye kiwanda cha unga anasema wanaweza kuwa Dubai nyengine akikusudia taifa la kibiashara la Ghuba ambalo limefanikiwa kupunguza utegemezi wake kwa mafuta.

 • Tarehe 12.03.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHlU
 • Tarehe 12.03.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHlU
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com