Bayern Munich yatunisha misuli katika Bundesliga | Michezo | DW | 10.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Bayern Munich yatunisha misuli katika Bundesliga

Bayern Munich  yatanua  misuli  yaonesha  nani mbabe  wa ligi  ya  Ujerumani,Bundesliga  kwa  kuinyoa  Borussia Dortmund  bila  maji  katika mchezo  wa  28 wa ligi.

Bundesliga Bayern München vs Borussia Dortmund Ribery (picture-alliance/Promediafoto/M. Deines)

Mchezaji Franck Ribbery wa Bayern Munich akishangiria pamoja na David Alaba bao la kwanza dhidi ya Dortmund

Ulikuwa  mwisho  wa  juma  wa  kilio  na  masikitiko makubwa kwa  makamu  bingwa  wa  ligi  ya  Ujerumani Bundesliga  Borussia  Dortmund  baada  ya  kugaragazwa na  mabingwa  watetezi  wa  ligi  hiyo Bayern  Munich  siku ya  Jumamosi  kwa  kukandikwa  mabao  4-1  katika uwanja  wa  Allianz Arena  mjini  Munich. Bayern inaongoza ligi  hiyo kwa  pointi  10 kutoka  timu  inayoifuatia  RB Leipzig , wakati  timu  ya  tatu  inayoifuatia  Bayern   ni TSG  Hoffenheim   na  Borussia  Dortmund  ikiwa  katika nafasi  ya  nne.  Kocha  wa  bayern Carlo Ancelotti  baada ya  mchezo  huo  alisema  tu  kwamba  kila  kitu  kilikuwa sawa  na  sasa  tunaisubiri  Real Madrid  katika  mchezo wa  Champions League  hapo  Jumatano.

Nae  mshambuliaji  wa  Bayern  Munich Arjen Robben  ambaye aliisumbua  sana  safu  ya  ulinzi  ya  Dortmund  na hatimaye  kutia  saini  yake  kwa  bao  safi  la  3  alikuwa  na  haya  ya  kusema .

"Ulikuwa  mchezo  mzuri  sana. Unakuwa  ndani  ya mchezo  huo, na kuonekana. Nijisikia  raha sana. Mimi  si kijana  tena, na  ninapaswa  kufurahia  mchezo. Leo kila kitu kilikuwa  kizuri."

Bayern München vs Borussia Dortmund Arjen Robben Tor (Reuters/M. Dalder)

Arjen Robben akipachika bao la 3 kwa Bayern dhidi ya Dortmund

Kwa  bao  la  dakika  za  mwisho  RB Leipzig , sio  tu ilishinda  mchezo  wake  dhidi  ya  Bayer 04  Leverkusen kwa  bao  1.0  lakini  pia  imeimarisha  nafasi  yake  ya kufuzu  moja  kwa  moja  kucheza  katika  ligi  ya mabingwa  barani  Ulaya Champions League  msimu  ujao , ikiwa  ni  timu  iliyotokea  daraja  la  pili  msimu  huu. Kocha wa  Leipzig  Ralph Hasenhüttel  anathibitisha  hilo.

"Naam , hii  ndio sababu  ya  sisi kuja  hapa uwanjani. Kwasababu tunataka  kushuhudia  mchezo  kama  huu, kama kocha, timu  na  pia  mashabiki. Hizi  ndio  hisia  za kandanda. Mna mchezaji  mmoja  pungufu  uwanjani  na mnashinda  na  hasa  katika  dakika  za  mwisho. Huu  ni wakati , maalum  wenye  utamu  wa  aina  yake. Kwetu  sisi ilikuwa  siku ya  ushindi  muhimu sana."

Deutschland Leipzig gegen Leverkusen (Getty Images/AFP/R. Michael)

Mchezaji wa RB Leipzig Yussuf Poulsen akifunga bao la ushindi dhidi ya Leverkusen

FC Kolon  kwa  mara  nyingine  tena  imeteleza  mbele  ya adui  yake anayemuogopa  kila  mara. Kolon  imeshindwa kutamba  nyumbani  kwa  kukandikwa  mabao  3-2  na Borussia  Moenchengladbach  katika  Derby  ya  eneo  la mto Rhine  siku  ya  jumamosi, ushindi  ulioisukuma  timu hiyo  kuikaribia  Kolon  kwa  kutofautiana  nayo  kwa  pointi moja  tu  katika  nafasi  ya  nane , wakati  Kolon  iko  nafasi ya  saba  katika  msimamo  wa  ligi  ya  Bundesliga  msimu huu,  na  kuporomoka  kutoka  nafasi  ya  kucheza  katika ligi  ya  Ulaya  msimu  ujao.

Kocha  wa  Gladbach Dieter Hecking  amesema  timu  yake ilikuwa  na  nia  ya  ushindi  tangu  mwanzo.

"Uliweza  kuona  kuanzia  dakika  ya  mwanzo , kwamba tulitaka  kushinda. Tulitaka  kushinda, bila  kujali  vile Kolon inavyoweza  kuhimili. Tulitaka  kila  wakati  kuonesha , kwamba  kidogo  uwezo  wetu  ni  mkubwa , ambao unatuwezesha  kushinda. Hilo timu  yangu  ililifanya  vizuri."

Bundesliga Borussia Mönchengladbach vs Bayern München - Trainer Dieter Hecking (Getty Images/Bongarts/M. Hitij)

Kocha wa Borussia Moenchengladbach Dieter Hecking akitoa maelekezo uwanjani

Hamburg SV  kwa  mara  ya  tatu  mfululizo  imeweza kushinda  mchezo  wake wa  nyumbani  kwa  kuiangusha  1899 TSG  Hoffenheim  kwa  mabao  2-1  na  kujikongoja  kidogo kidogo  kutoka  katika  eneo  la  hatari  ya  kushuka  daraja , licha  ya  kwamba  kitisho  hicho  hakijamalizika.

Schalke 04  nayo  ikaonesha  kwamba uwezo  wake unadhoofishwa  msimu  huu  na  matatizo  ya  wachezaji wake  wengi  kuwa  majeruhi , kwa  kuicharaza  VFL Wolfsburg  kwa  mabao 4-1 , wakati  Hertha Berlin iliishinda Augsburg  na  kuisababishia  timu  hiyo kuingia katika  hofu  ya  kushuka  daraja.

Bundesliga Schalke Wolfsburg Caligiuri, (picture-alliance/AP Photo/M. Meissner)

Wachezaji wa Schalke 04 wakishangiria bao katika mchezo dhidi ya Wolfsburg

Augsburg  iko sasa katika  nafasi  ya  16, ikiwa  pamoja  na  FC Ingolstadt na Damstadt ikishika  mkia. Njia  ya  damstadt  kuelekea daraja  la  pili  iko  nyeupe  baada  ya  jana  Jumapili kukandikwa  mabao  3-2  na Ingolstadt  ambayo inajaribu kujinasua  kutoka  hatari  ya  kushuka  daraja , ikiwa  na pointi  28 , moja  tu chini  ya  Augsburg , na FSV Mainz zote  zikiwa  na  pointi  29. Lakini  pia  VFL  Wolfsburg yenye  pointi 30  haiko  salama  sana.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / APE

Mhariri:Iddi Ssessanga