Bayern Munich yalipiza kisasi kwa Inter Milan | Michezo | DW | 24.02.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bayern Munich yalipiza kisasi kwa Inter Milan

Mario Gomez alifunga bao la ushindi kunako dakika ya mwisho na kuipa Bayern Munich ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Inter Milan

default

Mario Gomez kulia akimtoka mlinda mlango wa Inter Milan Julio Cesar na kupachika bao pekee na la ushindi kwa Bayern Munich.

Katika mechi hiyo iliyochukuliwa kama marudio ya fainali ya michuano hiyo ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, mlinda lango wa Inter Milan Julio Ceaser aliutema mkwaju wa Arjen Robben, aliyeufyatua kutoka umbali wa mita 22 na kumpa nafasi Gomez kuutumbukiza wavuni.

Bayern ambao walishindwa na Inter Milan mabao 2-0 mjini Madrid msimu uliopita, walionekana kuwa hatari katika kipindi kizima cha mechi hiyo ya kwanza katika hatua hii ya mtoano. Frank Ribbery na Arejn Robben walishuhudia mikwaju yao ikigonga mwamba wa goli.

Inter Milan pia walipata nafasi za kuweza kufunga, huku Luiz Gustavo akikosa nafasi mbili za wazi.Lakini Samuel Eto ndiye aliyekuwa hatari zaidi kwa upande wa Inter.

Katika mchuano mwingine, Olympique Marseille na Manchester United zilitoka suluhu bin suluhu katika mechi iliyofanyika katika dimba la Stade Veledrome nchini Ufaransa.

Kulikuwa na nafasi chache mno za kufunga, huku safu za ulinzi za timu zote mbili zikiwa thabiti. Matokeo hayo sasa yanaashiria kivumbi kikali kitakachoshuhudiwa katika mkondo wa pili uwanjani Old Trafford kule Uingereza, baada ya viongozi hao wa Ligi ya Primia kushindwa kufunga bao la ugenini.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri:Josephat Charo