Bayern Munich wasuasua | Michezo | DW | 22.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Bayern Munich wasuasua

Mabingwa Bayern Munich watarudi katika hali ngumu ya Bundesliga baada ya kuchuana na Lazio katika Champions League hapo Jumanne.

Bayern waliipoteza mechi yao ya dhidi ya Eintracht Frankfurt 2-1 na hii inafuatia ile sare ya magoli matatu waliyolazimishwa na vibonde Arminia Bielefeld na kutokana na hili uongozi wao katika Ligi Kuu ya Ujerumani umepunguzwa hadi pointi mbili. Hii ni baada ya timu iliyo katika nafasi ya pili RB Leipzig kupata ushindi wa 3-0 walipokuwa wakichuana na Hertha Berlin.

Baada ya kushindwa huko mlinda lango Manuel Neuer amesema hatua yao ya kukubali magoli kwa urahisi ndiyo imewaponza.

"Kutoka mwanzo hatukuwa tayari, hatukuwa mchezoni, hatukuwa wakakamavu vya kutosha na hiyo ni hatari sana kwa mpinzani kama huyu, kisha tukakubali mabao mawili na hivyo ndivyo ilivyokuwa dhidi ya Bielefeld. Kwa bahati mbaya kipindi cha pili ndio tulianza kujizatiti na kuonyesha uwezo wetu hasa," alisema Neuer.

Rose anachukua lawama ya kushindwa Gladbach

Bayern ambao kwa sasa wana pointi 49 watakuwa wanapambana na timu iliyo karibu na eneo la kushushwa daraja FC Cologne siku ya Jumamosi huku Wolfsburg walio kwenye nafasi ya tatu watakuwa wanakwaana na hertha Berlin kisha Borussia Dortmund wacheze na Arminia Bielefeld. RB Leipzig watakuwa wenyeji wa Borussia Mönchengladbach ambao mwishoni mwa wiki iliyopita walishangazwa na Mainz walipofungwa 2-1.

Kocha wao Marco Rose amesema lawama ya kushindwa huko anaichukua yeye kutokana na kauli aliyoitoa wiki iliyopita aliposema kwamba mwishoni mwa msimu atahamia Borussia Dortmund, jambo lililowaghadhabisha mashabiki wa klabu hiyo.

Rose Marco Trainer Team Borussia Moenchengladbach

Kocha wa Borussia Mönchengladbach Marco Rose

"Kwangu mimi ilikuwa wazi kwamba nataka kuwa hapa na kufanya kazi kikamilifu kuanzia siku ya kwanza, ila kila mmoja anaweza kuondoka. Maneno niliyoyasema hayakutusaidia uwanjani na matokeo tuliyoyapata uwanjani hayamsaidii yeyote. Nachukua jukumu la kushindwa kwetu leo, nachukua jukumu la jinsi walivyocheza vijana wangu ila nafikiri wiki ijayo tuna mechi ngumu ambayo tunastahili kuonyesha kwamba bado tupo," alisema Rose.