Kocha Marco Rose aahidi kutoondoka na wachezaji nyota | Michezo | DW | 17.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Kocha Marco Rose aahidi kutoondoka na wachezaji nyota

Kocha wa Borussia Moenchengladbach Marco Rose ameahidi kutochukua wachezaji nyota wowote wa Gladbach anapoelekea kuinoa Borussia Dortmund msimu ujao.

Siku ya Jumatatu siri kubwa iliwekwa wazi, Kocha wa Gladbach Marco Rose ataondoka na kuelekea Dortmund msimu ujao.

"Niliamua kuchukua kazi hiyo ya kusisimua huko Borussia Dortmund. Haikuwa rahisi," alisema Rose katika mkutano na waandishi wa habari.

Kocha Rose mwenye umri wa miaka 44 ameiongoza Gladbach kwenye hatua ya mchujo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo watachuana na Manchester City siku ya Jumatano ya tarehe 24.2.2021 katika mchezo wao wa duru ya kwanza ya timu 16 bora utakaofanyika huko Budapest.

Chini ya usimamizi wake, Gladbach imeshinda mechi dhidi ya vilabu vya juu vya Bundesliga kama vile Bayern Munich, RB Leipzig na Dortmund nyumbani msimu huu huko Borussia Park na kutoka sare na Real Madrid katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Wachezaji kama mshambuliaji Marcus Thuram na kiungo wa kati Florian Neuhaus chini ya ukufunzi wake Rose wamefanikiwa kuitwa kujiunga na timu za mataifa yao.

Wakati anaondoka Salzburg mnamo 2019, aliwachukua beki wa kulia Stefan Lainer na kiungo wa kati Hannes Wolf kutoka klabu hio ya Austria hadi Gladbach.

Alipoulizwa kama historia itajirudia atakapojiunga na Dortmund Rose amesema, "Ikiwa nimesema sitachukua mchezaji kwenda naye Dortmund, basi sitampeleka mchezaji Dortmund. Nimemaliza."

Borrusia Moenchengladbach italazimika kutafuta benchi la ukufunzi zima kwa sababu Rose anaondoka na wasaidizi wake wote watatu kuelekea Dortmund. Lakini kwa sasa anashikilia kuwa ataendelea kuinoa Gladbach kwa ari kuelekea mechi kati ya Gladbach na Dortmund ya kuwania Kombe la shirikisho la Ujerumani DFB Pokal mnamo Machi 2.

"Hakuna kilichobadilika katika mtazamo wangu kwa mwajiri wangu, bado ni chanya. Ninahusika kwa asilimia 100," amesisitiza Rose.

Katika jedwali la Bundesliga, Gladbach na Dortmund zote zina pointi 33, pointi sita kabla ya kufuzu kwa michuano ya mabingwa barani Ulaya.

Taarifa za kuondoka kwake zimewakasirisha mashabiki wa Gladbach huku kukiwekwa mabango ya kumkejeli Rose nje ya uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo.

Kocha Jesse March, anayesimamia sasa Red Bull Salzburg na Florian Kohfeldt wa Werder Bremen ni miongoni mwa wanaoweza kuchukua nafasi ya Rose huko Gladbach.

 

AFPE