1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern ina mlima mkubwa wa kukwea dhidi ya Barcelona

11 Mei 2015

Champions League inarejea tena uwanjani wiki hii, baada ya mashabiki kushuhudia mapambano ya vuta nikuvute wiki iliyopita katika nusu fainali mkondo wa kwanza

https://p.dw.com/p/1FOFT
Championsleague Halbfinale Barcelona gegen Bayern München
Picha: Reuters/Pfaffenbach

Kesho Jumanne mashabiki watashuhudia pambano la vuta nikuvute nguo kuchanika kati ya Bayern Munich na FC Barcelona baada ya mchezo wa kwanza Barcelona kuonesha uwezo mkubwa na kushinda kwa mabao 3-0 nyumbani Camp Nou.

Kocha wa Bayern Munich Pep Guardiola ameahidi kwamba timu yake itapambana , katika juhudi zake ambazo ni karibu na kutowezekana ili kuinyima Barcelona nafasi ya nane kuingia fainali ya kinyang'anyiro hicho.

Bayern inatafuta kufanya miujiza katika uwanja wa allianz arena baada ya kipigo hicho cha mabao 3-0 Jumatano iliyopita. Hakuna timu iliyoweza kubadilisha matokeo ya mabao 3-0 katika nusu fainali ya kombe lolote la Ulaya.

Pep Guardiola nach Champions League Spiel München vs Barcelona
Pep Guardiola anakabiliwa na shinikizo kubwaPicha: Getty Images/AFP/J. Lago

"Tunafahamu kwamba itakuwa kazi ngumu mno , lakini hatujakata tamaa," amesema mshambuliaji wa Bayern Thomas Mueller.

Lakini kocha wa Bayern Guardiola , ambaye alikuwa kocha ya Barca , anasisitiza kwamba kikosi chake kinapasa kuweka ndoto yao hai.

"Naamini hali halisi, hii ndio njia pekee ya kuweza kushinda ," amesema raia huyo wa Uhispania , ambaye amekionya kikosi chake kuwa kuna hatari ya kuvurugwa iwapo hawataweza kuwadhibiti washambuliaji nyota wa Barcelona. Nae kocha wa Barcelona Luis Enrique anakataa kuamini Bayern watasalim amri bila ya kupambana. " Niliona wakifungwa na Augsburg, wamefungwa lakini walicheza kwa dakika 70 na wachezaji 10 tu uwanjani. Tutateseka sana mjini Munich, amesema Louis Enrique.

Siku ya Jumatano itakuwa zamu ya Real Madrid ikiikaribisha Juventus Turin ambayo katika mchezo wa kwanza nyumbani iliambulia ushindi wa mabao 2-1.

Wakati huo huo kocha wa Bayern Munich Pep guardiola amekanusha uvumi unaozagaa kwamba anahmia katika kilabu cha Manchester City msimu ujao , akisema atamaliza mkataba wake na mabingwa hao wa Ujerumani. "Msimu ujao nitakuwa hapa na hilo ndio naweza tu kusema ," amesema Guardiola , ambaye ameshinda vikombe viwili msimu uliopita na ubingwa wa ligi msimu huu. Vyombo kadhaa vya habari vimeripoti jana Jumapili kuwa Manchester City imefikia makubaliano ya awali na Guardiola.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / dpae / ape / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga