Barua pepe za Hillary Clinton kuchunguzwa upya | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Barua pepe za Hillary Clinton kuchunguzwa upya

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema itaanzisha uchunguzi mpya kuangalia kama waziri wake wa zamani Hillary Clinton alifanya makosa kwa kutumia anuani binafsi ya barua pepe katika mawasiliano ya kikazi.

Hillary Clinton: Kivuli cha barua pepe kinamwandama.

Hillary Clinton: Kivuli cha barua pepe kinamwandama.

Msemaji wa wizara hiyo John Kirby amesema watakuwa na uwazi mkubwa iwezekanavyo, lakini hawatajiwekea muda wa mwisho wa kukamilisha mchakato huo. Kirby amesema hatua hiyo ni baada ya kuhitimishwa kwa uchunguzi wa wizara ya sheria, ambao ulisema hakutakuwapo mashitaka yoyote dhidi ya Hillary Clinton.

Kirby vile vile amekanusha shutuma kwamba wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marakeni ina utamaduni wa uzembe kuhusu masuala ya mawasiliano.

''Madai ya kwamba wizara hii kama taasisi, ina utamaduni wa uzembe, hatukubaliano nayo, na kama alivyosema mkurugenzi wa FBI, hayo siyo kweli, wala hayakuwa sehemu ya uchunguzi na mapendekezo yaliyotokana na uchunguzi huo.'' Amesema Kirby.

Clinton ayaponyoka mashitaka

Mkurugenzi wa FBI James Comey amehojiwa na kamati ya uchunguzi ya bunge

Mkurugenzi wa FBI James Comey amehojiwa na kamati ya uchunguzi ya bunge

Mwanzoni mwa wiki hii shirika la upelelezi la Marekani, FBI lilipendekeza Bi Clinton ambaye ananuia kugombea urais wa Marekani katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu, asifunguliwe mashitaka yoyote, kutokana na kutumia kwake anuani binafsi ya barua pepe kwa masuala nyeti ya kikazi, wakati alipokuwa waziri wa mambo ya nchi za nje kati ya mwaka 2009 na 2013. Pendekezo hilo liliheshimiwa na wizara ya sheria.

Ingawa uamuzi huo ulimpa ahueni Bi Clinton, mkurugenzi wa FBI James Comey alisema bayana kwamba Clinton alifanya uzembe kupita kiasi katika mawasiliano hayo ya barua pepe.

Pendekezo la kutomfungulia mashitaka Hillary Clinton liliwachukiza warepublican, akiwemo Donald Trump ambaye anatarajiwa kuwa mpinzani wa Bi Clinton katika uchaguzi wa Novemba, wakisema kiongozi huyo amekwepa mkondo wa sheria kutokana na hadhi yake kama mwanasiasa wa ngazi ya juu.

FBI kibanoni

Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden na Hillary Clinton

Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden na Hillary Clinton

Jana Mkurugenzi wa FBI alilazimika kulitetea pendekezo la kutomshitaki Bi Clinton, katika kamati ya bunge inayohusua uchunguzi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje John Kirby hakutoa maelezo zaidi kuhusu uchunguzi huu mpya, mbali na kusema utakuwa na uwazi mkubwa,na utaheshimu majukumu yao kisheria.

Mkurugenzi wa FBI amesema miongoni mwa barua pepe 30,000 ambazo Hillary Clinton alizikadhi kwa shirika lake, 100 zilikuwa na taarifa nyeti. Nyingine 2000 zilipandishiwa hadhi ya unyeti, na kufanywa nyaraka za siri.

Wakati sakata hilo likiendelea kuvuma, Bi Hillary Clinton ameungana na makamu wa rais wa Marekani Joe Biden katika kampeni jimboni Pennsylvania, katika kuhamasisha umoja ndani ya chama cha Democratic, kabla ya mkutano wake mkuu utakaoanza tarehe 25 mwezi huu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com