FBI yamnusuru Clinton kushitakiwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

FBI yamnusuru Clinton kushitakiwa

Mgombea mtarajiwa wa urais wa Marekani wa chama cha Democratic Hillary Clinton amenusurika hatari ya kushitakiwa kutokana na namna alivyoshughulikia barua pepe zenye taarifa nyeti akiwa waziri wa mambo ya nchi za nje.

Hillary Clinton amepumua pumzi ya ahueni baada ya kunusurika kushitakiwa

Hillary Clinton amepumua pumzi ya ahueni baada ya kunusurika kushitakiwa

Ripoti ya shirika la upelelezi nchini Marekani FBI ambayo ilitolewa jana, imemshutumu Hillary Clinton kufanya ''uzembe kupindukia'' kuhusu barua pepe hizo, lakini ikapendekeza asishitakiwe.

Uamuzi huo umempa ahueni mgombea huyo wa chama cha Democratic, na kuwapokonya wapinzani wake wa chama cha Republican turufu ya kubadilisha mkondo wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa Novemba kwa manufaa yao.

Hakukuwa na dhamira ya kufanya uhalifu

Mkurugenzi wa FBI, James Comey

Mkurugenzi wa FBI, James Comey

Akiisoma ripoti ya shirika analoliongoza, mkurugenzi mkuu wa FBI James Comey alimshutumu kwa kutumia anuani yake binafsi ya barua pepe katika mawasiliano yaliyohusisha taarifa nyeti. Hata hivyo, aliongeza kuwa hawakubaini makusudi ya kufanya uhalifu.

''Tukirejelea uchunguzi wetu katika kushughulikia taarifa nyeti, hatukuona sababu inayounga mkono hatua ya kumfungulia mashitaka. Visa vyote vilivyopelekwa mahakamani hapo awali vilikuwa na mseto wa dhamira ya kutumia vibaya taarifa za siri, na kufanya makusudi kuzivujisha katika hali ambayo inaashiria kukosa uaminifu kwa Marekani, au juhudi za kukwamisha mkondo wa sheria. Hayo hatukuyaona hapa.'' Amesema Comey.

Warepublican wajawa na ghadhabu

Ripoti hiyo haikuwapendeza warepublican. Spika wa baraza la wawakilishi Paul Ryan, mrepublican mwenye cheo cha juu zaidi cha kuchaguliwa, amesema ripoti ya FBI haieleweki, na kutaka ripoti nzima ichapishwe, na kusema huenda mkurugenzi wa shirika hilo akaitwa katika bunge kujieleza mbele ya kamati ya ukaguzi, ili kutoa maelezo zaidi.

Donald Trump, asema mfumo wa Marekani umeghubikwa na hila

Donald Trump, asema mfumo wa Marekani umeghubikwa na hila

Donald Trump mrepublican anayetarajiwa kupambana na Bi Clinton katika uchaguzi wa rais mwezi Novemba, pia ameishambulia vikali ripoti hiyo, na kwenda mbali zaidi akidai mfumo wa sheria wa Marekani umegubikwa na hila.

Alisema, ''Muda wote nimekuwa nikihisi Hillary Clinton atakwepa kushitakiwa kwa mienendo yake ya kihalifu na yenye hatari kubwa, kwa sababu nilijua, na nimejua siku zote, na inasikitisha, kwamba mfumo wetu umejaa hila, umegubikwa na hila, na umenunuliwa. Ni aibu.''

Obama amumwagia sifa Clinton

Wakati warepublican wakilalamika, upande wa Hillary Clinton umefanya hima kuendelea na kampeni, ukisema imeridhika na ripoti ya FBI.

Kwa mara ya kwanza Rais Barack Obama ameambatana na Bi Clinton katika kampeni hiyo, wakisafiri pamoja kwenye ndege ya rais, kwenda katika jimbo la North Caroline, ambapo amesifu tabia za mgombea huyo aliyewahi kuwa waziri wake wa mabo ya nchi za nje.

Obama amesema hakuna mtu yeyote, mwanaume au mwanamke, aliyewahi kuwa na sifa murua za kuwa rais wa Marekani, kuliko Hillary Clinton.

Trump amempiga vijembe Obama akimwita rais asioyejua anachokifanya katika kuambana na Bi Clinton, akisema hatua yake hiyo ni kama tamasha tu la kitamaduni.

Maoni ya watu katika mitandao ya kijamii baada ya ripoti ya FBI kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya kumkosoa Bi Clinton, kuliko kumuunga mkono.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe

Mhariri: Caro Robi

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com