1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lapitisha azimio kuhusu Syria

12 Julai 2020

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuwezesha kuendelea kutolewa huduma za msaada wa kiutu nchini Syria, taifa ambalo limeharibiwa kwa vita.

https://p.dw.com/p/3fB0s
New York UN Sicherheitsrat Sondersitzung Syrien
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/AA/T. Coskun

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuwezesha kuendelea kutolewa huduma za msaada wa kiutu nchini Syria, taifa ambalo limeharibiwa kwa vita.

Azimio hilo limepitishwa baada ya wajumbe wake kukubali shinikizo la Urusi la kufunga moja ya njia mbili zinazotumiwa kuingia kwenye taifa hilo lililoharibiwa kwa vita.

Nord-Syrien Tel Tamer | humanitäre Krise
Picha: DW/K. Zurutuza

Baada ya wiki ya migawanyiko na duru saba za upigaji kura, baraza hilo limepitisha pendekezo lililowasilishwa kwa pamoja kati ya Ujerumani na Ubelgiji na kuruhusu kutumiwa kwa eneo la Bb al-Hawa kama njia ya kuingiza misaada nchini Syria katika kipindi cha mwaka mmoja unaokuja.

Azimio hilo limepitishwa kwa kura 12 kati ya 15 za wajumbe wa Baraza la Usalama huku Urusi, China na Jamhuri ya Dominica zikijizuia kupiga kura.

Idhini ya kuendelea kupeleka misaada nchini Syria, utaratibu ambao umekuwepo tangu mwaka 2014, ilifikia kikomo Ijumaa usiku baada ya Moscow na Beijing kutumia kura za turufu kurefusha muda na Baraza hilo pia kupinga pendekezo mbadala lililotolewa na Urusi.

Matumaini ya kuelea kutolewa msaada 

UN-Sicherheitsrat verlängert Syrienhilfe eingeschränkt
Picha: picture-alliance/AP/S. Grits

Kuidhinishwa kwa pendekezo hilo la Ujerumani na Ubelgiji, eneo la Bab al-Hawa lililopo kwenye mpaka wa kaskazini magharibi ya Syria na Uturuki litasalia wazi kwa mwaka mmoja hadi Julai 10, 2021.

Hali hiyo itaruhusu msaada wa kiutu unaohitajika sana kuendelea kuingizwa na kuwafikia mamilioni ya wasyria wanaoishi kwenye jimbo la Idlib, kitovu cha uasi na eneo ambalo serikali ya Syria haina udhibiti.

Kwa wiki kadhaa, Urusi, mshirika muhimu wa Syria imekuwa ikishinikiza kufungwa kwa njia ya Bab al-Salam inayoelekea mkoa wa Allepo kaskazini ya Syria.

 Urusi inalenga kukomesha njia ya sasa ya utoaji wa msaada wa Umoja wa Mataifa nchini Syria ambayo huingia kwa kupitia Uturuki hadi kwenye maeneo ambayo hivi sasa hayako chini ya udhibiti wa serikali ya mjini Damascus

Mataifa ya Ulaya na Marekani yamekuwa yakishiniza kuendelea kuwepo kwa maeneo mawili ya kuendelea kuingiza msaada.