Marekani yahimiza msaada upelekwe Sudan
29 Machi 2024Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield alisema pande zinazopigana zote zimevuruga operesheni za utoaji misaada na kupuuzilia mbali wito wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kukomesha mara moja uhasama.
Kabla ya maadhimisho ya mwaka mmoja wa mzozo wa Sudan, Thomas-Greenfield alisema, "Hali nchini Sudan inabaki kuwa janga na inaendelea mbaya," aliwaambia waandishi habari. "Watu wanakufa njaa."
Vita vilizuka nchini Sudan mnamo Aprili 15, 2023 kati ya jeshi la Sudan SAF na kundi la wapiganaji wanamgambo wa RSF. Umoja wa Mataifa unasema watu takriban milioni 25 - nusu ya idadi jumla ya wakazi wa Sudan - wanahitaji msaada, kiasi milioni 8 wamelazimika kuyakimbia makazi yao na karibu milioni tano huenda wakakabiliwa na baa la njaa katika miezi ijayo.
Jeshi la Sudan lakwamisha upelekaji misaada
Thomas-Greenfield amelituhumu jeshi la Sudan kwa kukwamisha msaada kutoka Chad kuingia eneo la Darfur Magharibi mwa Sudan, linalodhibitiwa na wapiganaji wa RSF - na ameielezea hali halisi kuwa ya maisha na kifo.
"Katika kambi ya Zamzam huko Darfur Kaskazini mtoto hufariki kila baada ya muda wa masaa mawili. Wataalamu wanatahadharisha kwamba katika wiki na mizi inayokuja zaidi ya watoto 200,000 huenda wakafa njaa," alisema, na kulitolea wito jeshi la Sudan SAF kuufungua tena mpaka kikamilifu mara moja.
"Kama hawataufungua mpaka, baraza la usalama lazima lichukue hatua ya haraka kuhakikisha msaada utakaoyaokoa maisha unapelekwa na kusambazwa, ikiwa ni pamoja na mkakati wa mipakani, ikilazimika," alisema Thomas-Greenfield.
Baraza la usalama limeamuru operesheni za namna hiyo hapo kabla - kwa miaka tisa liliruhusu upelekaji wa msaada wa kibinadamu kutoka nchi jirani kuepelekwa kwa mamilioni ya watu katika maeneo yaliyokuwa kwa kiwango kikubwa chini ya udhibiti wa upinzani nchini Syria.
Soma pia: Jeshi la Sudan lapinga kusitisha mapigano, RSF ikikaribisha wito huo
Marekani inasema pande zinazohasimiana nchini Sudan zimefanya uhalifu wa kivita. Serikali ya mjini Washington inaitazama Aprili 18 kama siku ya kuanza tena mazungumzo ya kutafuta amani ya Sudan huko nchini Saudi Arabia, mjumbe maalumu wa Marekani kwa ajili ya Sudan, Tom Perriello, alisema siku ya Jumanne.
Kati ya watu 10,000 na 15,000 wameuliwa katika mji mmoja pekee katika eneo la Darfur Magharibi mwaka uliopita katika machafuko ya kikabila kati ya wapiganaji wa kikosi cha RSF na wanamgambo wa muungano wa kiarabu, kwa mujibu wa ripoti ya wafuatiliaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na shirika la habari la Reuters mnamo mwezi Januari mwaka huu.
(rtre)