1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza jipya la mawaziri Ufaransa kukutana

18 Mei 2017

Uungaji mkono wa chama kipya cha rais wa Ufaransa Emmanuel Macron unaongezeka kabla uchaguzi wa wabunge mwezi ujao, na haya ni kwa mujibu wa kura ya maoni.

https://p.dw.com/p/2dAFV
Frankreich Emmanuel Macron Amtseinführung
Rais mpya wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Getty Images/AFP/F. Mori

Matokeo ya kura hiyo ya maoni yalitolewa Alhamis, jambo linaloongeza uwezekano wa kuungwa mkono na wabunge katika mikakati yake ya kuleta mabadiliko. Baraza la mawaziri aliloliteua rais huyo mpya Jumatano, linakutana kwa mara ya kwanza Alhamis.

Macron mwenye umri wa miaka 39 na ambaye ni rais mpya wa Ufarana  aliwapa kazi za uwaziri wahafidhina, wasosholisti na wanasiasa wapya ambapo kwa kufanya hivyo, aliyaunganisha mapengo yaliyopo na kuongeza kuungwa kwake mkono. Baraza hilo jipya la mawaziri litakutana kwa mara ya kwanza hii leo.

Katika mahojiano katika redio moja nchini Ufaransa, Waziri Mkuu Edouard Philippe alipuuza madai kwamba serikali hiyo ya Macron iliyo na mchanganyiko, ni mbwembwe za kisiasa tu na akasema kusonga mbele ndiyo kauli inayoiweka pamoja serikali hiyo.

Baraza hili la mawaziri ni matayarisho ya uchaguzi wa bunge

"Kwa kweli ni serikali iliyounda kwa ajili ya kudumu, wakati kura za ubunge zinapokaribia, serikali hii bila shaka ni muhimu na ndiyo itakayoamua kila kitu kitakachotokea baada ya hapo," alisema Philippe, "lakini serikali iko hapa kuongoza. Iko hapa kutayarisha mwamko mpya, iko hapa kubuni kitu, iko hapa kuweka miradi mahali pake."

Domique Reynie ni mchambuzi wa siasa katika taasisi ya mafunzo ya siasa ya Paris, "hii ni serikali ya mawasiliano kwa uchaguzi wa bunge. Ni matayarisho ya uchaguzi wa bunge," alisema Dominique, "mawaziri hao wanaweza kufanya kazi zao za kila siku, lakini hawawezi kufanya maamuzi makubwa. Hawawezi kupitisha miswada yoyote."

Frankreich Marine Le Pen nach der zweiten Runde der französischen Präsidentschaftswahlen 2017
Chama cha Marine Le Pen cha National Front kimepuuza mabadiliko ya MacronPicha: picture alliance/dpa/AP Photo/M. Euler

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Front, kimepuuza mabadiliko hayo aliyoyafanya Macron kikisema ni kiini macho tu  na kimemshutumu rais huyo kwa kutumia tena wanasiasa wa zamani kutoka mrengo wa kushoto na kulia.

Asilimia 32 ya wapiga kura watakipigia chama cha Macron

Lakini kura ya maoni ya Harris, ilitoa matokeo ya uchunguzi wake na kupata kwamba chama cha Republic on the Move, pamoja an wandani wake, kinatarajiwa kushinda idadi kubwa ya kura katika raundi ya kwanza ya uchaguzi huo wa bunge Juni 11.

Asilimia 32 ya wapiga kura 4,600 waliojisajili walipoulizwa, walisema wanapanga kukipigia kura chama cha Macron katika uchaguzi huo. kura hiyo ya maoni inaonesha kuongezeka uungaji mkono wa Macron kwa alama tatu zaidi ikilinganishwa na kura ya maoni iliyofanywa Mei tarehe 7, siku ambayo Macron alimshinda kiongozi wa mrengo wa kulia Marine Le Pen na kunyakua urais.

Chini ya mfumo wa upigaji kura wa Ufaransa, iwapo hakuna mgombea atakayeshinda kura zinazohitajika kutangazwa mshindi katika raundi ya kwanza ya upigaji kura katika kura za bunge, wagombea wanaoongoza wanakwenda katika raundi ya pili itakayokuwa Juni 18.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu