Barack Obama: Kwaheri Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Barack Obama: Kwaheri Berlin

Rais Barack Obama wa Marekani amekutana kwa faragha na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwa chakula cha jioni baada ya kuwasilii Berlin katika ziara yake ya mwisho barani Ulaya akiwa rais wa Marekani.

Mkutano huo wa chakula cha jioni ulifanyika katika Hoteli ya Adion ambayo iko karibu kabisa na eneo la kihistoria la Brandenburg Gate mjini Berlin ambapo Obama na ujumbe wake watakuwapo hadi kesho Ijumaa.

Haikuweza kufahamika kitu gani hasa viongozi hao wawili wamekijadili juu kwamba yumkini masuala waliyojadili ni pamoja na kuchaguliwa kwa Donald Trump katika uchaguzi wa rais kuchukuwa nafasi ya Obama na mzozo wa Syria.

Mazungumzo zaidi yanatarajiwa kufanyika baadae leo hii katika ofisi ya Kansela Merkel.Obama aliwahi kumpongeza Merkel kuwa ni mshirika wa kuaminika na alitetea msimamo wake wa kushughulikia mzozo wa wakimbizi ambao ulimgharimu kisiasa kwa kushuka kwa umashuhuri wake nchini Ujerumani.

Mashaka juu ya Trump

Deutschland Barack Obama und Angela merkel in Berlin (picture-alliance/dpa/EPA/M. Sohn)

Rais Barack Obama wa Marekani na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakati wa chakula cha jioni mjini Berlin.

Licha ya kwamba ziara yake hiyo ilipangwa kabla ya hata ya uchaguzi wa rais wa Novemba nane safari hii ya kimataifa ya kuaga imegeuka kuwa safari ya kutuliza wasi wasi kufuatia ushindi wa Trump huku kukiweko na mashaka juu ya aina ya sera atakazofuata.

Trump alikuja kuungwa mkono kutokana na ahadi zake za kujenga ukuta katika mpaka wa Mexico na Marekani,kuwapiga marufuku kwa muda Waislamu kuingia nchini Marekani na kuikataa mikataba ya biashara ambayo amesema imewaumiza wafanyakazi wa Marekani.

Obama anapingana na misimamo hiyo na anapigania kubakisha mafanikio ya haiba yake kwa huduma za afya,mabadiliko ya tabia nchi na diplomasia kwa suala la silaha za nyuklia ambapo Trump anaahidi kuachana nayo.

Pongezi za Merkel kwa Trump kufuatia ushindi wake katika uchaguzi huo wa rais ziliandamana na tahadhari ambapo wakati akiahidi kumpa rais huyo mteule wa chama cha Republikan ushirikiano wa karibu katika mazungumzo yake na simu na kiongozi huyo amesisitiza ushirikiano huo utakuwa chini ya misingi ya maadili ya demokrasia.

Demokrasia ni ngumu

Griechenland Athen - Barack Obama (picture-alliance/AP Photo/P. M. Monsivais)

Rais Barack Obama wa Marekani akizungumza mjini Athens.

Akiwa mjini Athens nchini Ugiriki mahala kulikozaliwa demokrasia kabla ya kuwasili Ujerumani hapo jana Rais Obama amekiri kwamba demokrasia yumkini ikachukuwa muda,inaweza kukatisha tamaa, ni ngumu na inaweza kuwa ya fujo lakini hatimae ni bora zaidi kuliko mbadala wake.

 Obama alisema "Nchini Marekani na kila mahali nilipotembelea katika kipindi hiki cha miaka minane nimekutana na raia hususan vijana ambao wameamuwa kuwa na matumaini badala ya hofu,wanaoamini wanaweza kujenga hatima yao wao wenyewe,waliokataa kuikubali dunia kama vile ilivyo na kuazimia kuijenga upya kama inavyopaswa kuwa.Wamenishajiisha."

Hapo kesho Obama anatarajiwa kukutana na viongozi wa Ufaransa, Uhispania,Italia na Uingereza na inatarajiwa suala la kurefusha vikwazo dhidi ya Russia litajadiliwa kwa kuingilia masuala ya Ukraine na uwezekano wa vikwazo vipya kwa mshambulizi yake ya mabomu nchini Syria.


Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa /DW

Mhariri : Gakuba Daniel

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com