Aung San Suu Kyi aapishwa kuwa mbunge | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Aung San Suu Kyi aapishwa kuwa mbunge

Kiongozi wa upinzani wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, leo ameapishwa kuwa mbunge. Kuapishwa kwake kulichelewa kwa muda wa wiki moja baada ya Suu Kyi awali kukataa kula kiapo kwa sababu hakubaliani na katiba ya nchi.

Aung San Suu Kyi akiapishwa

Aung San Suu Kyi akiapishwa

Aung San Suu Kyi amekubali kula kiapo baada ya kuwekewa shinikizo na chama chake cha National League for Democracy NLD pamoja na wafuasi wake. Chama hicho kilikuwa kikisubiri kwa hamu kiongozi wake achukuwe nafasi yake bungeni na kuanza kufanya kazi. Suu Kyi pamoja na wenzake kutoka chama cha NLD leo waliapa kulingana na katiba ya mwaka 2008 na hivyo wameahidi kuilinda katiba. Lakini katiba hiyo ililaumiwa sana na wapinzani katika kampeni za uchaguzi zilizoendelea hadi tarehe 1 Aprili mwaka huu kwani inaupa utawala wa kijeshi madaraka mengi, ikiwemo haki ya utawala huo kuchukua robo ya viti vilivyopo bungeni.

Ban Ki-moon alipomtembelea Suu Kyi Myanmar

Ban Ki-moon alipomtembelea Suu Kyi Myanmar

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, katika ziara yake nchini Myanmar alimsifu Suu Kyi kwa kubadili msimamo wake na kukubali kuapishwa kuwa mbunge. "Wakati mwingine wanasiasa wanakuwa na mawazo tofauti kuhusu masuala fulani lakini kiongozi wa kweli anaonyesha kwamba anaweza kubadili mtazamo wake kwa ajili ya kuwafaidisha watu wake na taifa lake. Na hiki ndicho alichokifanya."

Suu Kyi ataka kubadili katiba

Hata hivyo, Aung San Suu Kyi alieleza kwamba hali ya kubadili mtazamo si mkakati mpya wa upande wa upinzani. "Wakati wote tulifahamu kwamba ni lazima tuwe tayari kubadili msimamo wetu kama tunataka kufikia malengo yetu, hasa katika kipindi ambacho tulikuwa tunagandamizwa," alisema kiongozi huyo. "Hivyo kuwa tayari kubadili msimamo si jambo jipya kwetu. Ilikuwa sehemu ya ujuzi wetu wa kisiasa katika miaka 23 iliyopita."

Myanmar bado inatawaliwa na wanajeshi

Myanmar bado inatawaliwa na wanajeshi

Muda atakaoutumia Aung San Suu Kyi kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni bado haijafahamika. Ahadi mojawapo ilikuwa kubadili katiba ya nchi yake iliyotungwa na utawala wa kijeshi. Suu Kyi alieleza kwamba daima amekuwa na imani juu ya mafanikio na kuongeza kwamba katika siasa ni lazima mtu awe na matumaini.

Viongozi wa chama tawala cha USDP, ambao mara nyingi wamekuwa wakimpinga Suu Kyi, wameeleza kwamba uwepo wake bungeni utakuwa na faida kwa upande wa upinzani ambao kwa sasa una nguvu ndogo sana ya kisiasa.

Mwandishi: Udo Schmidt/Elizabeth Shoo/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com