1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Amina: Malkia shujaa wa Zazzau

Yusra Buwayhid
6 Februari 2020

Katika wakati ambapo kila kitu kikiendeshwa na wanaume , malkia Amina wa Zazzau aliibuka. Shujaa wa kijeshi kutoka kabila la Hausa. Aliongoza jeshi kubwa, lilonyakuwa maeneo mengi na kuweza kuupanua ufalme wake.

https://p.dw.com/p/3XFS8
DW African Roots | Queen Amina of Zazzau

Amina: Malkia shujaa wa Zazzau

Vipi unaweza kwa kifupi kulieleza jina la Amina wa Zazzau?

'Amina, mwanamke kama mwanaume!' Hivyo ndiyo alivyokuwa akielezwa Amina. Kila kitu alichokifanya kama malkia kilizidi kile walichokifanya watangulizi wake wa kiume. Na sasa jina lake linatumika kuwakilisha nguvu na uwezo wa mwanamke.

Amina aliishi lini na wapi?

Inaaminika Amina alizaliwa katika karne ya 16 lakini wasomi wanakinzana juu ya tarehe sahihi ya kuzaliwa kwake. Aliishi katika mji unaojulikana leo kama Zaria, jimbo la Kaduna, Nigeria.

Amina atakumbukwa kwa lipi?

  • Anakumbukwa sana kama malkia shujaa anayeheshimiwa.

  • Alitawala kwa miaka 34 na kupanua ufalme wake katika maeneo mengi aliyoweza kuyakamata.

  • Alifungua pia njia za biashara na inaaminika alianzisha ulimaji wa njugu za kola katika maeneo aliyokuwa akiyadhibiti.

  • Sultan wa pili wa Sokoto, Mohammed Bello, ambaye pia alikuwa mtoto wa Usman dan Fodio, mpiganaji maarufu aliyeeneza dini ya Kiilslam, alimuandika kwa mara ya kwanza katika kitabu chake 'Infaku'l Maisuri'. Kulingana na kitabu hicho, Amina alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha utawala kama unavyojulikana sasa katika jamii za Hausa, na pia alikuwa na kipaji cha kipekee cha uongozi.

    Amina: Malkia shujaa wa Zazzau

Je, kuna masuala gani yenye utata yanayomhusu Amina?

  • Kuna baadhi wanaodai kwamba Amina ni hadhithi tu na kwamba mtu wa aina hiyo hakuwa kuishi Nigeria. Lakini kuna ushahidi unaothibitisha uwepo wake. Moja wapo ni kuta alizozijenga kuzungushia miji aliyoitawala. Halikadhalika, bado kuna magofu ya sehemu lilipokuwepo kasri lake pamoja na viwanja vya mafunzo ya kijeshi huko Zaria.

  • Ingawa hakuwa na watoto, kuna madai kuwa vizazi vya ndugu zake bado viko hai na ni miongoni mwa watu wenye hadhi katika eneo hilo.

  • Sababu na mahali pa kifo chake bado ni suala la ubishani, lakini wengi wanakubaliana kwamba aliuawa katika vita vya Atagara, eneo linalojulikana sasa kama jimbo la Kogi, kaskazini ya kati Nigeria.

    DW African Roots | Queen Amina of Zazzau
    DW Asili ya Afrika, Malkia Amina wa Zazzau

Amina ankumbukwa vipi nchini Nigeria na kwengineko?

  • Sehemu tofauti na taasisi za kaskazini mwa Nigeria zimepewa jina la Amina. Moja wapo ni shule ya sekondari ya serikali katika jimbo la Kuduna, Chuo cha Malkia Amina. Kuna pia dahalia za wanafunzi wa kike zinazoitwa Ukumbi wa Malkia Amina katika Chuo Kikuu cha Ahmadu Bello, Zaria, na Chuo Kikuu cha Lagos.

  • Mhusika katika kipindi cha televisheni ya Marekani 'Xena: Bintimfalme Shujaa' inasemekana anatokana na Amina, bintimfalme na baadaye malkia wa Zazzau.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na taasisi ya Gerda Henkel.