1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Algeria bingwa wa AFCON.

Lilian Mtono
20 Julai 2019

Algeria imefanikiwa kunyakua ubingwa wa kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuiondoa Senegal kwenye fainali za michuano hiyo ilipoifunga bao 1-0.

https://p.dw.com/p/3MMfk
Ägypten Africa Cup of Nations 2019 | Finale Algerien gegen Senegal | Jubel
Picha: Reuters/M. Abd El Ghany

Bao hilo la ushindi lililopatikana katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo na lilifungwa katika dakika ya pili na mshambuliaji wa Algeria Baghdad Bounedjah.

Shuti kali la Bounedjah lililosababisha bao hilo pekee la ushindi katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa International Stadium, lilitokana na shambulizi lililofanywa katika dakika za mapema kabisa za mchezo huo.

Goli hilo la sekunde ya 79 ni la kwanza kufungwa katika dakika za mwanzoni za michuano ya mataifa ya Afrika kwa karibu miaka 39, na kuifanya Algeria kuwa mabingwa kwa mara ya pili wa michuano hiyo na mara ya kwanza tangu mwaka 1990.

Senegal walipewa penalti katika kipindi cha pili cha mchezo, lakini penalti hiyo ilifutwa baada ya uamuzi wa mwamuzi wa VAR. Mwamuzi wa mchezo huo Mcameroun Alioum Alioum alimwadhibu mchezaji wa Algeria Adlane Geudioura baada ya kuunawa mpira, lakini alibadilisha uamuzi baada ya kuwasiliana na mwamuzi msaidizi wa video. VAR imetumika kwa mara ya kwanza kwenye michuano hii.

Ägypten Africa Cup of Nations 2019 | Finale Algerien gegen Senegal
Kocha wa Senegal Aliou Cisse akimtuliza mchezaji wake Ismaila Sarr anayelia baada ya kutolewa kwenye fainali za AFCONPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

Senegal kwa mara nyingine wanaondoka mikono mitupu, baada ya kulikosa kombe hilo mwaka 2002.

Hata hivyo Senegal ilionekana kuutawala mchezo huo huku ikijaribu kutengeneza nafasi za kufunga. Lakini kukosekana kwa mlinzi wa kati anayecheza na klabu ya Napoli, Kalidou Koulibaly anayetumikia adhabu kuliidhoofisha Senegal na Salif Sane anayekipiga na klabu ya Schalke 04 ya Ujerumani aliyerejea kwenye nafasi yake baada ya kupona majeraha pia hakuwa na msaada mkubwa kwenye kikosi chake.

Pamoja na kuanza vyema mchezo huo na kuwafanya watulie na kuendelea kuutawala mchezo lakini Senegal hawakufanikiwa kuwatisha Algeria ambao walionekana kutumia muda mwingi kulinda bao hilo licha ya kwamba walikuwa na mshindi wa michuano ya klabu bingwa Ulaya ama Champions, Sadio Mane aliyekiongoza kikosi hicho.

Ägypten Africa Cup of Nations 2019 | Finale Algerien gegen Senegal | Jubel
Kocha wa Algeria Djamel Belmadi akiwa amebebwa juu juu akipongezwa na wachezaji wakePicha: Reuters/M. Abd El Ghany

Senegal haijawahi kushinda michuano hiyo ya Mataifa ya Afrika. Kocha wa Senegal Aliou Cisse alijikuta katika wakati mwingine mgumu baada ya kukosa penalti iliyoikosesha Senegal ubingwa katika fainali za mwaka 2002.

Algeria, ilikuwa na haki ya kuibuka mshindi wa michuano hiyo baada ya kushinda katika kila mechi ikiwa ni pamoja na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Senegal katika hatua ya makundi. Kapteni wa Algeria Riyadh Mahrez anajiongezea kombe kibindoni baada ya klabu anayochezea ya Manchester City inayoshiriki ligi la PL kunyakua ubingwa wa ligi hiyo msimu uliopita.

Wachezaji wa Algeria pamoja na kocha wao Djamel Belmadi walipiga magoti na kufanya dua huku wakiwa wamewageukia mashabiki wao baada ya kipyenga cha mwisho. Kocha huyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Algeria ameongoza mbio za kikosi hicho hadi ubingwa baada ya kukichukua chini ya mwaka mmoja uliopita.