1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

Al-Shabaab yadai kuhusika na shambulio mjini Mogadishu

10 Juni 2023

Kundi la kigaidi la Al-Shabab limedai kuhusika na shambulio kwenye hoteli moja maarufu katika mji mkuu Mogadishu jana Ijumaa ambalo limesababisha majeruhi ya takriban watu saba.

https://p.dw.com/p/4SPcO
ARCHIV | Somalia Mogadischu | Sicherheitskräfte nach Anschlag
Maafisa wa usalama wakishika doria katika hoteli ya Hayat mjini Mogadishu baada ya watu wenye silaha kuivamia.Picha: Farah Abdi Warsameh/AP Photo/picture alliance

Shirika la habari la serikali limeandika kwenye mtandao wao wa Twitter kuwa vikosi vya usalama vinaendesha oparesheni ya kuwasaka wapiganaji wa Al-Shabab waliohusika na shambulio hilo.

Shirika hilo limeripoti kuwa, "raia wengi" wameokolewa wakiwa hai kutoka hoteli hiyo ya Pearl huku mapigano yakiendelea usiku kucha. Hakuna ripoti zozote za vifo vilivyotokea kutokana na shambulio hilo.

Soma pia: Al-Shabaab washambulia kambi ya Umoja wa Afrika, Somalia

Shambulio katika hoteli ya Pearl ilioko ufukweni mwa bahari lilitokea mapema jana jioni.

Mkurugenzi wa kampuni ya Amin inayomiliki magari ya kubebea wagonjwa Abdikadir Abdirahman amesema wamepokea watu saba waliojeruhiwa katika shambulio hilo.

Somalia Militants Twitter
Wapiganaji wa Al-Shabab wakifanya mazoezi ya kijeshi viungani mwa mji mkuu Mogadishu.Picha: picture alliance / AP Photo

Kundi la Al-Shabab lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda limesema katika taarifa kuwa, wapiganaji wake wamefanikiwa kuingia katika hoteli ya Pearl ilioko ufuoni mwa bahari na kwamba bado wanaudhibiti.

Kundi la Al-Shabab lenye makao yake nchini Somalia linajulikana kwa kufanya mashambulizi kwenye hoteli za kifahari na maeneo yenye kutembelewa na watu mashuhuri mjini Mogadishu, aghalabu huanza kwa kufanya shambulio la bomu la kujitoa mhanga.

Soma pia:Uganda yathibitisha kuuawa wanajeshi wake 54 wa jeshi la kulinda Amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia. 

Hoteli ya Pearl iko karibu na ubalozi wa Uturuki na hutembelewa sana na viongozi na maafisa wakuu wa serikali ya Mogadishu.

Mwishoni mwa mwezi Mei, wapianaji wa Al-Shabab walishambulia kambi ya jeshi la Uganda kilomita 130 kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu na kuwaua wanajeshi 54.