1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Ajali ya treni yauwa takribani watu 280

Sudi Mnette
3 Juni 2023

Watu wasiopungua 280 wamekufa na wengine 900 wamejeruhiwa baada ya treni mbili za abiria kugongana huko katika Jimbo la Odisha nchini India

https://p.dw.com/p/4S96H
BG Zugunglück in Indien
Picha: Satyajit Shaw/DW

Mapema Jumamosi, serikali ya India ilisema ajali hiyo inaingia katika rekodi za ajali mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja. Mtendaji Mkuu wa Jimbo la Odisha,Pradeep Jena amesema idadi ya waliokufa kufuatia ajali hiyo ya Ijumaa inatarajiwa kuongozeka.

Aliongeza kuwa zaidi ya magari 200 ya kubebea wagonjwa yalikwenda katika eneo la ajali katika wilaya ya Balasore ya Odisha na madaktari wa ziada 100, ikiwa kuwaongezea nguvu wengine 80 ambao tayari walikuwepo katika eneo la tukio.

Hali ya simanzi katika eneo la tukio.

Zugunglück in Indien
Jitahada ya uokozi wa manusura nchini IndiaPicha: Press Trust of India/dpa/picture alliance

Vidio zilizopatikana katika eneo la tukio zilionesha waokoaji wakiwa katika jitihada zao za kuwasaka manusura katika baadhi ya mabehewa huku kukitapakaa vilio vya baadhi yao wakiomba msaada. Shuhuda mmoja ambae alikuwepo katika eneo hilo amenukuliwa na Shirika la Habari la Uingereza-Reuters akisema "Nilikuwa pale katika eneo la ajali, nimeweza kuona kutapakaa kwa damu, viungo vilivyovunjika na watu wanakufa katika mazingira hayo."

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa moja usiku, siku ya Ijumaa wakati treni ya shirika "Howrah Superfast Express" iliyokuwa ikitokea Bangalore kuelekea Hawrah, Bengal Magharibi kugongana na treni nyingine ya shirika "Coromandel Express" iliyokuwa ikitokea Kalkata kwenda Chennai.

Taarifa zinazochanganya kuhusu chanzo cha ajali.

Mamlaka nchini India imekuwa ikitoa taarifa zenye kupishana kuhusu kiini cha ajali hiyo. Hadi wakati huu hakujawa na majawabu ya treni ipi iliacha reli yake na kuigonga nyingine. Na hadi wakati huu haijatoa taarifa ya kina kuhusu chanzo cha ajali hiyo.

Operesheni ya kabambe ya utafutaji wa miili ya watu na uokoaji imeanzishwa, ikihusisha mamia ya wafanyakazi wa idara ya zima moto, maafisa wa polisi na mbwa wa kunusa.Timu za Kikosi cha Kitaifa cha Kukabiliana na Maafa zimepelekwa pia kwenye eneo la tukio.

Soma zaidi:Watu 22 wauawa katika ajali ya boti India

Muda mfupi baada ya ajali hiyo Ijumaa, mamia ya vijana walijipanga nje ya hospitali ya serikali Odisha kuchangia damu. Kwa mujibu wa na  Shirika la Reli la India watu takribani milioni 13 wanasafiri kwa kutumia treni kila siku. Lakini mtandao unaoendeshwa na serikali umekuwa ukikabiliwa na changamoto za kiusalama na miundombinu yake kuzeeka.