Afrika katika magezeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 07.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magezeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameuzingatia mgogoro wa wafanyakazi wa migodi nchini Afrika Kusini. Gazeti la die "tageszeitung linasema hakuna matumaini ya kuutatua mgogoro huo hivi karibuni

Wafanyakazi wa migodini nchini Afrika Kusini

Wafanyakazi wa migodini nchini Afrika Kusini

Gazeti la "Süddeutsche "linazungumzia juu ya mauaji ya wafanyakazi 34 waliopigwa risasi na polisi. Kichwa cha habari cha makala ya gazeti hilo kinasema: Sheria ya enzi za utawala wa kibaguzi.

Gazeti hilo linaarifu kwamba "Polisi wa Afrika Kusini wamewapiga risasi na kuwaua wafanyakazi wa migodini 34, lakini ni wafanyakazi 270 waliokabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kudhamiria." Gazeti la "Süddeutsche" limemkariri aliekuwa kiongozi wa tawi la vijana la chama cha ANC, Julius Malema, akisema "dunia nzima imeona jinsi polisi walivyowaua wafanyakazi." Hata hivyo mashtaka ya mauaji yaliyokuwa yanawakabili wafanyakazi hao yametupiliwa mbali na wafanyakazi waliotiwa ndani sasa wameachiwa.

Jarida la "Focus"linasema katika makala yake kwamba mambo yanasonga mbele barani Afrika. Jarida hilo linauzungumzia mji wa Lagos nchini Nigeria. Linaeleza kuwa "picha waliyokuwanayo watu wengi ya mji wa Lagos ni ile ya vurumai, uchafu na hatari. Jarida la "Focus" linasema ni kweli kwamba mambo hayo yapo katika mji wa Lagos. Lakini kuna picha nyingine; ile ya watu wanaondesha magari, na wapita njia wenye simu za mkononi. Katika mji huo watu wanafanya biashara badala ya kufa njaa, na badala ya kuuana wanaujenga mji wao."

Jarida la Focus linazungumzia juu ya maendeleo ya barani Afrika kwa jumla. Limemkariri Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi "Julius Berger-International, Wofgang Goetsch, akiwashauri watu waachane na picha zinazoonyesha maafa tu barani Afrika. Mkurugenzi huyo amekaririwa akisema kwamba anaingiwa uchungu akiona watu barani Ulaya wakishikilia habari juu ya dhiki tu barani Afrika.!

Jarida la Focus linatilia maanani kwamba watu milioni 315 sasa wana kipato kinachovuka dola mbili kwa siku barani Afrika. Waafrika milioni 120 wana kipato kinachovuka dola nne kwa siku. Afrika inang'ara, linasema jarida la "Focus".

Gazeti la "der Freitag" linatupasha habari zaidi juu ya mpiga picha kutoka Vietnam anaeshi mjini Berlin. Mpiga picha huyo Kien Hoang Le ameliambia gazeti la "der Freitag" kwamba hapo awali alilijua bara la Afrika kutokana na taarifa za vyombo vya habari vya nchi za magharibi. Kien Hoang Le amesema bara hilo lilikuwa linaonyeshwa katika vyombo hivyo kama doa la uchafu .Wakati wote vyombo hivyo vinatoa taarifa juu ya umasikini, maafa na vita tu.

Mpiga picha huyo alitumia muda wa nusu mwaka kusafiri kwa pikipiki barani Afrika. Amesema, baada ya muda mfupi, picha aliyokuwa nayo juu ya Afrika ilikuwa inabadilika kila siku. Ameliambia gazeti la "der Freitag" kwamba hali halisi ni tofauti kabisa. Amezungumza na Waafrika wa tabaka la kati na ameweza kutambua kwamba hao ni watu waliojengeka vizuri kitaaluma. Kien Hoang aliezaliwa Vietnam mnamo mwaka wa 1987, anafanya kazi kama mpiga picha kwa ajili ya magazeti, majarida na asasi zisizo za kiserikali. Alisafiri kwa piki piki nchini Malawi, Rwanda, Kenya na Tanzania.

Taarifa juu ya mpiga picha huyo inaonyesha kwamba siyo ajabu watu kutoka Ulaya wanaenda kutafuta maisha bora barani Afrika. Gazeti la "Financial Times Deutschland" linaarifu katika makala yake kwamba Wareno wanarejea Afrika.Gazeti hilo linaeleza kuwa maalfu ya Wareno wanatafuta maisha bora nchini Angola.

Nchi hiyo ambayo hapo awali lilikuwa koloni la Ureno, sasa imekuwa imara kiuchumi kutokana na mafuta. Mmoja wa Wareno hao ni Rui Ferreira. Kutokana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi ulioikumba nchi yake, Ureno, Ferreira ameamua kuihamishia kampuni yake nchini Angola. Gazeti la "Financial Times Deutschland" limeripoti katika makala yake kwamba Wareno 500 wanawasili nchini Angola kila mwezi.

Mwandishi:Mtullya Abdu / Stumai George/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Miraji Othman