1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Bintou Keita DRC yakumbwa na purukushani

16 Aprili 2021

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Congo Bintou Keita amewasili Beni, ambako alikutana na wajumbe wa mashirika ya kiraia. Mazungumzo yao yaligubikwa na purukushani

https://p.dw.com/p/3s8BQ
DR Kongo Treffen Bintou Keita und Félix Tshisekedi
Picha: Giscard Kusema/Kommunikationsdienst DR Kongo

Polisi waliwatawanya waandamanaji waliokuwa njiani kukutana na Bintou Keita mjini Beni. Vijana hao wa vuguvugu la mabadiliko la Lucha waliandamana kuelekea makao makuu ya Monusco katika kata ya Boikene, kuitikia mwaliko wa Bintou Keita, mwakilishi maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Congo.

Vijana hao hawakufanikiwa kukutana na mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa, kwani walitawanywa na jeshi la polisi, lililokuwa linatekeleza amri ya gavana wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini Nzanzu Kasivita, aliyepiga marufuku maandamano katika mkoa wake.

Purukushani kati ya vijana wa Lucha na jeshi la polisi, hazikuwazuia wajumbe fulani wa mashirika ya kiraia kukutana kwa mazungumzo na Bintou Keita.

Baada ya kukutana kwa mazungumzo na wajumbe hao, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Congo Bintou Keita, alizungumza na waandishi wa habari, ambapo alilaani uharibifu wa mali unaofanywa wakati wa maandamano dhidi ya tume ya Umoja wa mataifa, pamoja na mashirika ya kiutu katika eneo hili.

Aidha Keita alisikitika kuhusu mauwaji yanayofanywa na waasi katika wilaya ya Beni, na kasema kwamba, kuna vikosi maalumu vitakavyofanya kazi bega kwa bega na jeshi la Congo katika operesheni dhidi ya waasi.

Wajumbe wa mashirika ya kiraia wasubiri kutekelezwa kwa ahadi za Keita

DR Kongo Treffen Bintou Keita und Félix Tshisekedi
Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Congo Bintou Keita akiwa na raid wa DRC Félix TshisekediPicha: Giscard Kusema/Kommunikationsdienst DR Kongo

Wajumbe wa mashirika ya kiraia, pamoja na kumsikiliza mwakilishi maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Congo, wanasema kwamba, wanasubiri kuona Monusco inatekeleza kwa vitendo, ahadi za Keita, katika kurudisha usalama kwenye eneo hili.

Mazungumzo baina ya mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Congo, yanaonekana kuwa hayakuzaa matunda kwani,maandamano pamoja na mgomo vinaendelea katika eneo hili.

soma zaidi:Mwakilishi Maalum wa katibu mkuu wa UN afanya ziara DRC

Vijana waandamanaji,walitishia kushambulia makao makuu ya Monusco katika kata ya Boikene, bila ya kufanikiwa,kwani askari polisii walifanikiwa kuwatawanya.

Milio ya risasi imekuwa ikisikika katika kata mbalimbali za mji wa Beni,ambako vijana wameweka vizuizi barabarani.

Mgomo na maandamano dhidi ya Monusco vimeingia siku yake ya kumi na mbili leo, na vitasitishwa baada ya siku kumi na nane,kwa mjibu wa tangazo la vuguvugu la vijana, lililoitisha mgomo huo.

Mwandishi: John Kanyunyu DW Beni