1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky awashukuru wanajeshi wake

9 Juni 2023

Jeshi la Ukraine limesema asubuhi ya leo kwamba limedungua makombora manne na kuyazuia mashambulizi 10 ya droni yaliyofanywa na Urusi usiku wa kuamkia leo huku rais Volodymyr Zelensky akiyashukuru majeshi yake.

https://p.dw.com/p/4SNG3
Picha hii inamuonyesha rais Volodymyr Zelensky akimpongeza na kumkabidhi medali mwanajeshi wa jeshi la maji wa Ukraine, Mei 23, 2023.
Rais Volodymyr Zelensky ameendelea kuwapongeza wanajeshi wake kwa kujitoa msitari wa mbele kupambana na uvamizi wa Urusi.Picha: Ukrainian Presidential Press Service/Handout via REUTERS

Jeshi la Ukraine linatoa taarifa hiyo, huku rais Volodymyr Zelensky akiyashukuru majeshi yake kwa kuhakikisha wanakabiliana vilivyo katika vita vyake dhidi ya Urusi na kudokeza kuwa mashambulizi bado yanaendelea.

Rais Volodymyr Zelensky aidha amesema amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na makamanda walioko katika maeneo kunakoshuhudiwa mapigano makali zaidi, ambayo ni pamoja na mkoa wa Donesk na kuwashukuru wanajeshi kwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri. Amesema hayo kupitia ujumbe wa video alioutoa akiwa mafichoni jana Alhamisi.

Amesema "Ninawasiliana mara kwa mara na jeshi letu. Makamanda wa Khortytsia, Tavria na wale wote wanaohusika katika maeneo yenye mapigano makali zaidi. Eneo la Donetsk: vita kali sana. Lakini kuna matokeo, na ninamshukuru kila mtu anayehakikisha matokeo haya. Bakhmut, wamefanya kazi nzuri. Hatua kwa hatua Ninamshukuru kila mpiganaji wetu."

Zelensky aidha amelaani vikali mashambulizi yaliyofanywa katika eneo la Kherson, akiituhumu Urusi kwa kushambulia maeneo ambako waathriwa wa mafuriko walikuwa wakihamishwa, baada ya shambulizi la daraja lililosababisha mafuriko makubwa. Amesema magaidi wa Urusi wanajaribu kuchochea hali mbaya, waliyoisababisha wenyewe kutokana na mauaji waliyoyafanya.

Wakazi wa eneo hilo wakisafiri kwa mashua kufuatia mafuriko huko Kherson mnamo Juni 8, 2023 baada ya bwawa la kituo cha kuzalisha umeme cha Kakhovka, kushambuliwa.
Shambulizi dhidi ya bwawa la Kakhovka limesababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na mafuriko.Picha: ALEKSEY FILIPPOV/AFP/Getty Images

Huko mjini Kyiv, taarifa za jeshi la anga zimesema Urusi imetumia droni 16 na makombora sita katika mashambulizi ya hivi karibuni na kuwajeruhi watu wanane, wawili kati yao wakiwa katika hali mbaya baada ya makombora mawili kuanguka kwenye eneo la kiwanda na sehemu ya kuoshea magari.

Mashariki mwa mkoa wa Dnipropetrovsk, mashambulizi ya droni na makombora yaliharibu majengo mawili ya makaazi ya watu na bomba la gesi, ingawa meya wa eneo hilo Serhiy Lysak amesema hakukua na vifo. Shambulizi hilo lilifuatiwa na mashambulizi mengine ya angani yaliyofanywa kote nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na Kyiv, usiku mzima wa jana.

Ukraine yakataa kuzungumzia mashambulizi yake ya kushtukiza.

Katika hatua nyingine, Urusi imeripoti makabiliano makali katika jimbo la Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine mapema leo baada ya hapo jana afisa wa ngazi za juu wa kijeshi wa Urusi kumwarifu rais Vladimir Putin kwamba wiki hii wamemefanikiwa kuzuia majaribio ya mara kadhaa ya jeshi la Ukraine, ambayo Moscow inayataja kama sehemu ya jaribio kubwa la mashambulizi ya kushtukiza ya Ukraine, yaliyoanza siku ya Jumapili.

Rais Volodymyr Zelensky akizungumza na wakaazi wa eneo lililokumbwa na mafuriko huko Kherson, Juni 8,2023.
Uharibifu wa bwawa la kuzalisha umeme la Kakhovka umeibua kitisho kikubwa zaidi cha mafuriko na kuwalazimisha raia kuondoja kwenye makazi yao.Picha: Ukraine Presidency/AFP

Ukraine hata hivyo imekataa kuzungumzia juu ya mashambulizi hayo ya kushtukiza ambayo yamesubiriwa kwa muda mrefu, na badala yake imeituhumu Urusi kwa kusambaza uongo kuhusu mashambulizi hayo. Gazeti la Marekani la New York Times liliwanukuu maafisa watatu wa ngazi za juu wa Marekani waliosema mashambulizi hayo yako mbioni.

Msemaji wa kundi la wapiganaji la Vostok la Urusi amesema wameteketeza vifaru 13 vya Ukraine kwenye mapigano hayo ya Zaporizhzhia na vinane huko Donesk. Hata hivyo shirika la habari la Reuters, halikuweza kuthibitisha hayo.

Taarifa nyingine kutoka Kyiv zinasema idara zake za usalama wa ndani zimenasa mazungumzo ya simu yaliyothibitisha juu ya kundi la watu kutoka Urusi waliohujumu bwawa la kuzalisha umeme la Kakhovka nchini humo. Idara ya Usalama ya Ukraine, SBU imechapisha sauti ya kama dakika moja na nusu kwenye ukurasa wa Telegram, ambapo mwanaume mmoja alisikika akimwambia mwenzake kwamba WaUkraine hawakushambulia bwawa hilo, bali ni kundi la nchini humo lililotumika kuhujumu. SBU inamuelezea mwanaume huyo kuwa ni mwanajeshi wa Urusi, ambaye alilalama kwamba shambulizi hilo halikufanyika kama lilivyopangwa.