1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Xi, Putin wasifu 'enzi mpya' katika mahusiano yao

Bruce Amani
22 Machi 2023

Viongozi wa China na Urusi wamesifu kile walichokiita "enzi mpya" katika mahusiano yao, wakati wakiuonyesha umoja wao mjini Moscow. Rais Putin alizituhumu nchi za Magharibi kwa kukataa mpango wa Beijing wa kumaliza vita

https://p.dw.com/p/4P2j9
Russlands Putin führt Gespräche mit Chinas Xi in Moskau
Picha: SERGEI KARPUKHIN/AFP

China na Urusi ambazo zina hamu ya kukandamiza nguvu za Magharibi, zilielezea wasiwasi kuhusu utanuzi wa Jumuiya ya NATO barani Asia na kukubaliana kuimarisha ushirikiano ambao umeendelea kuwa wa karibu hata zaidi tangu Putin alianzisha uvamizi nchini Ukraine.

Akizungumza baada ya kukutana na Rais wa China Xi Jinping, Putin alisema yuko tayari kwa mazungumzo kuhusu Ukraine na kuusifu mpango wa China wa ajenda 12 kuhusu mzozo huo, unaojumuisha wito wa mazungumzo na kuheshimiwa uhuru wa mipaka ya nchi zote. Hata hivyo alisema nchi za Magharibi hazionekani kuwa tayari kuujadili mpango wa amani unaopendekezwa na China.

 John Kirby
Marekani inasema China haiaminiki kuwa mpatanishiPicha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Kyiv imeialika China kwa mazungumzo, na inasubiri jibu kutoka kwa Beijing. "Kuhusu maamuzi ya kimsingi, tulitoa kwa ulimwengu mpango wetu wa amani. Tuliialika China kuwa mshirika katika utekelezaji wa mpango wa amani. Tuliwasilisha mpango wetu kwa wahusika wote. Tunaialika China kwa mazungumzo. Tunasubiri jibu."

Marekani, hata hivyo, inasema haiioni China kuwa na uwezo wa kuwa mpatanishi asiyeegemea upande wowote. Msemaji wa Usalama wa Taifa John Kirby amewaambia waandishi Habari kuwa China imejizuia kukosoa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na imeendelea kununua mafuta ya Urusi hata wakati nchi za Magharibi zikiendelea kuiwekea vikwazo sekta ya nishati ili kuinyima Kremlin fedha za kugharamia vita. "Kwa hivyo sasa, ikiwa China inataka kuchukua jukumu la kujenga katika mzozo huu, basi wanapaswa kuishinikiza Urusi kuondoa wanajeshi wake kutoka Ukraine. Wanapaswa kumhimiza Rais Putin aache kulipua miji, hospitali na shule." kukomesha uhalifu wa kivita na ukatili na kumaliza vita leo."

Mwaka mmoja tangu Urusi kuivamia Ukraine

Ziara ya Xi mjini Moscow imeonekana kuwa ya kumpiga jeki Putin, ambaye anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu – ICC kuhusu tuhuma za kuwafukuza kinyume cha sheria Watoto wa Ukraine.

Katika siku ya pili ya ziara yake ya Moscow, Xi alisema mahusiano na Urusi yanaingia enzi mpya. Putin aliyaita mazungumzo hayo kuwa yenye maana na ya wazi na akasema Urusi, ambayo kwa kiasi kikubwa imetengwa na masoko ya Ulaya kwa sababu ya vikwazo, itaweza kutimiza mahitaji ya China yanayoongezeka ya nishati.

Nishati ni ajenda muhimu ya ziara ya Xi, na Putin alitangaza kuwa nchi hizo mbili zimefikia makubaliano ya bomba la gesi la Power of Siberia 2, litakaloiunganisha Siberia na kaskazini magharibi mwa China.

Katika taarifa ya Pamoja, viongozi hao wawili walizituhumu nchi za Magharibi kwa kudhoofisha usalama wa ulimwengu.

Ukraine | Japanischer Premierminister Fumio Kishida in Kiew
Kishinda alizuru Kyiv katika ziara ambayo haikutarajiwaPicha: Alina Yarysh/REUTERS

Ziara ya Xi mjini Moscow iliwkenda sanjari na ziara ambayo haikutarajiwa ya Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida mjini Kyiv. Kishida alikutana na Zelensky ambapo aliiahidi Ukraine msaada wa kifedha pamoja na msaada wa kiutu na matibabu.

Kishida, kiongezi pekee wa kundi la nchi tajiri ulimwenguni - G7 ambaye hakuwa amezuru Ukraine tangu Urusi ilipoanza uvamizi kamili nchini humo Februari 2022, alikuwa amekumbwa na shinikizo la kufanya ziara hiyo, wakati Japan ikijiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa kundi hilo Mei mwaka huu.

Nalo Shirika la Fedha la Kimataifa IMF limesema limefikia makubaliano na Ukraine la mpango wa mkopo kwa miaka minne wa karibu dola bilioni 15.6. Fedha hizo ni za kusaidia katika mazungumzo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya na kuijenga upya nchi hiyo iliyokumbwa na vita.

afp, reuters, dpa