Wimbi la mabadiliko Zimbabwe? | Matukio ya Afrika | DW | 08.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Wimbi la mabadiliko Zimbabwe?

Rais mpya wa Zimbabwe amefungua njia ya kuwepo mazingira huru ambayo hayajapata kuonekana katika nchi hiyo ambayo bado inapambana kujikwamua kutokana na utawala wa miaka 37 wa aliyekuwa rais Robert Gabriel Mugabe.

Hata hivyo kwa wengine wanamuona Mnangagwa anavuka mipaka wakati wengine wakimkosoa kwamba anachokifanya ni mbinu tu za kiini macho kuelekea uchaguzi wa kihistoria mwezi Julai.

Mnangagwa alipoingia madarakani baada ya kujiuzulu rais Robert Mugabe aliyeshinikizwa na jeshi kuondoka madarakani mwezi Novemba mwaka jana  aliahidi kuleta mageuzi. Wengi wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu mrithi huyo wa Mugabe ambaye alikuwa makamu wake kwa kipindi chote cha utawala wa Mugabe,wakitaka kuthibitisha ikiwa kweli anachokisema anakimaanisha.  Hatua za kukamatwa kwa wanaharakati wa kisiasa  na maafisa wa upinzani ambazo zilikuwa wakati mmoja zikionekana kuwa jambo la kila siku chini ya Mugabe,zimepungua kwa kiasi kikubwa. Upinzani umekuwa ukifanya mikutano ya kampeini bila ya kuingiliwa tafauti na hali ilivyokuwa wakati wa utawala wa Mugabe.Uhuru wa kujieleza umeimarika.Lakini Mnangagwa pia amewagusa wananchi wa taifa hilo ambalo kwa kiasi kikubwa ni la watu wenye misimamo wa kihafidhina wenye maamuzi fulani.

Hisia mseto kwa Wazimbabwe ​​​​​​​

Ishara za mabadiliko ni bayana nchini Zimbabwe. Mapema mwezi uliopita, mwanamuziki maarufu alirejea kutoka uhamishoni nchini Marekani na kuwatumbuiza maelfu ya raia wa nchi hiyo kwa muziki wake wa harakati za mapinduzi nje ya mji mkuu Harare.

Siku chache baadaye, maonesho ya sanaa ya kila mwaka yaliayoandaliwa Harare yaliruhusiwa kualika bendi ya muziki ambayo video zake zililipigwa marufuku kwasababu zilionekana kumdhihaki aliyekuwa rais Robert Mugabe.

Waandamanaji kwenye barabara za Harare

Waandamanaji kwenye barabara za Harare

Mnangagwa aliahidi mabadiliko ya kidemokrasia alipochukua hatamu za uongozi, Mugabe alipojiuzulu mwezi Novemba baada ya shinikizo za majeshi, umma pamoja na chama chake mwenyewe cha ZANU-PF.

Kasi ya kukamatwa kamatwa kwa wanaharakati wa kisiasa na wanachama wa upinzani katika utawala wa Mugabe sasa imepungua kwa kiwango kikubwa. Upinzani umekuwa ukiandaa mikutano ya hadhara bila ya kutatizwa na serikali kinyume na ilivyokuwa katika utawala wa Mugabe.

Uhuru wa kujieleza umepanuka, huku raia wa Zimbabwe wakikosoa serikali bila ya hofu hasa katika maeneo ya mijini. Maeneo ya vijijini mashirika yasiyokuwa ya serikali yangali yanaandikisha visa vichache vya viongozi wa vijiji kuwatisha wakazi wakitaka maelezo yao ya kupiga kura.

Siku ya Jumatano, Mnangagwa alikilaani chama chake kwa kutumia polisi kama mawakala wa kusimamia vituo vya kupiga kura wakati wa uchaguzi wa chama hicho. Mnangagwa amepata uungwaji mkono kama huo kutoka pande mbali mbali.

Lakini rais huyo mpya ambaye ameinadi  kauli mbiu kwamba  Zimbabwe inafungua milango kwa wawekezaji baada ya miaka kadhaa ya kuwa chini ya vikwazo vya kimataifa  kuhusiana na rekodi yake ya haki za binadamu pia amezigusa hisia za wananchi wa taifa hilo ambao kwa kiwango kikubwa ni wahafidhina wenye misimamo fulani. 

Zimbabwe imeruhusu kilimo cha bangi na ukahaba

Robert Mugabe aliyekuwa rais wa Zimbabwe

Robert Mugabe aliyekuwa rais wa Zimbabwe

Serikali yake imehalalisha kilimo cha  bangi kwasababu za kisayansi na matibabu. Aidha serikali hiyo imeruhusu makahaba kushiriki katika maonesho ya kimataifa ya kibiashara, hafla ambayo ilifunguliwa rasmi na Mnangagwa mwenyewe kama njia ya kuuelimisha umma kuhusu kazi zao na njia salama  ya kushiriki vitendo vya ngono.

Kwenye mitandao ya kijamii na mitaani na pia baadhi ya wanasiasa, wanamkosoa rais huyo kwa kuvuka mipaka ya uhuru. Aliyekuwa makamu wa rais Joice Mujuru na sasa ni kiongozi wa upinzani anasema kuwa serikali inatengeza mitego ambayo hatimaye itasambaratisha familia. Anoengeza kusema kuwa serikali inataka kuharibu vijana.

Wengine wanamuunga mkono rais wakisema kuwa kuna mafao ya kiuchumi watakayoleta makahaba pamoja na ukulima wa bangi katika taifa hilo ambalo wakati mmoja lilikuwa limepiga hatua.

Ukahaba nchini Zimbabwe ni jambo la kawaida lakini unaochukiwa kijamii na umepigwa marufuku, japo mahakama ya kikatiba mwaka 2015 iliamua kuwa ni makosa kwa wanawake kutiwa nguvuni kwasababu ya kujinadi kingono.

kwa kuhalalisha ukulima wa bangi, Zimbabwe imekuwa moja ya mataifa machache barani Afrika kufanya hivyo.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ap

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com