1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa 12 Afrika yapatiwa chanjo ya Malaria

6 Julai 2023

Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza jana kuwa litawasilisha dozi milioni 18 za chanjo ya malaria kwa Mataifa 12 ya Afrika ifikapo mwaka 2025.

https://p.dw.com/p/4TV25
Malaria-Bekämpfung in Afrika | Kenia | Impfstoff Mosquirix
Picha: Brian ONGORO/AFP

Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza jana kuwa litawasilisha dozi milioni 18 za chanjo ya malaria kwa Mataifa 12 ya Afrika ifikapo mwaka 2025. Mpango huo utaendeshwa kwa usaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF.

Kama sehemu ya mpango wa majaribio, chanjo hiyo ya Mosquirix (RTS,S), iliyotengenezwa na kampuni kubwa ya dawa ya Uingereza GSK, tayari imetolewa kwa zaidi ya watoto milioni 1.7 katika nchi tatu za Afrika ambazo ni Ghana, Kenya na Malawi.

Majaribio hayo yamedhihirika kuwa salama na yenye ufanisi, na nchi hizo tatu zitaendelea kupokea dozi pamoja na nchi zingine tisa zitanufaika na mpango huo. Nazo ni Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Liberia, Niger, Sierra Leone na Uganda.

Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema malaria inasalia kuwa moja ya magonjwa hatari zaidi barani Afrika, na kuua kila mwaka karibu watoto nusu milioni walio chini ya umri wa miaka mitano. Mnamo mwaka 2021, asilimia 96 ya vifo vya malaria duniani vilitokea barani Afrika.